29 August 2011

Bei ya mafuta yapungua tena

Na Grace Michael

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei elekezi ya mafuta ambapo kwa kipindi hiki yameshuka kwa kati ya asilimia 2.11 petroli, dizeli
asilimia 1.57 na mafuta ya taa asilimia 1.28.

Kutokana na hali hiyo, Petroli imeshuka kwa sh. 44.55 na itauzwa sh. 2,069. 58, dizeli kwa sh. 31.99 na itauzwa kwa sh 1,999.32 na mafuta ya taa yameshuka kwa sh. 25.62 hivyo yatauzwa kwa sh. 1,979.79.

Akitangaza bei hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Bw. Haruna Masebu, alisema kuwa hatua hiyo inatokana na kanuni ya kukokotoa bei za bidhaa za mafuta ya petroli ambazo zimekuwa zikitangazwa kila baada ya siku 14.

Alisema kuwa mabadiliko ya bei za mafuta yametokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na bei hizo katika soko la ndani zingeshuka zaidi endapo thamani ya shilingi ya Tanzania ingekuwa juu.

Hata hivyo alisema kuwa bei za rejareja na za jumla zingepanda zaidi endapo fomula ya zamani ingeendelea kutumika. Alisisitiza kuwa  kuwa EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta kwa kuwa zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa hizo.

“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa,” alisema Bw. Masebu.

Wakati huo mamlaka hiyo imevifungia vituo vitatu vya mafuta na kuvitaka kujieleza kwa nini visichukuliwe hatua zaidi kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya kuuza mafuta chini ya kiwango na kuzuia maofisa wa EWURA kufanya kazi yao.

Akizungumzia hilo, Bw. Masebu alisema kuwa vituo hivyo vimetakiwa kujieleza ndani ya siku saba kutokana na makosa yaliyofanyika.

Vituo hivyo ni Kobil Kigamboni Depot ambayo imefungiwa kwa kosa la kuuza mafuta yaliyo chini ya kiwango, Hass Magu ambayo nayo imefungiwa kwa kosa la kukata lakiri iliyokuwa imefungwa na EWURA na kisha kuendelea kuuza mafuta na Petro Mafinga Petrol Station ambayo nayo imefungiwa kutokana na kuwazua maofisa wa mamlaka hiyo kutekeleza jukumu lao kupima mafuta.

“Tutaendelea na ukaguzi katika vituo mbalimbali na wanaokiuka sheria zetu hatutasita kuwachukulia hatua stahili kwa mujibu wa sheria hivyo katika hili hatuna utani hata kidogo,” alisema Bw. Masebu.


1 comment:

  1. Kama bei mpya zinatangazwa kila baada ya siku 14 then kuwe na ufuatiliaji wa kuhakikisha kwamba bei zinaposhuka na wauzaji kweli washushe bei kama hilo hamliwezi basi hakuna haja ya kutuambia bei zimeshuka wakati wauzaji wanaendelea kutukamua.

    ReplyDelete