13 December 2012
RC Iringa aagiza makandarasi wasio na sifa wasipewe tenda
Na Eliasa Ally, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma, amewataka Wahandisi na Wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo, kuhakikisha hawatoi tenda kwa makandarasi wasio na fedha
pamoja na vifaa vya ujenzi wa barabara.
Alisema yapo malalamiko yanayotolewa na wananchi juu ya makandarasi wa aina hiyo kupewa tenda ya ujenzi wa barabara
hasa zilizopo vijijini ambazo zinajengwa chini ya kiwango
pamoja na miradi hiyo kuchelewa kukamilika.
Dkt. Ishengoma aliyasema hayo mkoani humo jana katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa na kusisitiza kuwa, kuanzia sasa marufuku kwa Mhandisi kutoa tenda kwa makandarasi wasio na sifa stahiki za kutengeneza barabara.
“Utendaji wao mbovu makandarasi wasio na sifa umechangia barabara nyingi zilizopo vijijini kushindwa kukamilika kwa
wakati na kudai hawajalipwa na halmashauri.
“Nishindwa kuelewa makandarasi hawa wanapewa tenda kwa vigezo gani, ninachojua mimi mkandarasi anayetaka tenda kwanza anapaswa kuwa na fedha za kuanza kutekeleza mradi husika, vifaa vya kutosha na usimamizi wa Mhandisi mwenye vyeti,” alisema.
Alisema kama makandarasi wabovu wataendelea kupewa tenda na halmashauri, watasababisha upotevu mkubwa wa fedha za Serikali pamoja na miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango hivyo upo uwezekano wa wananchi kuilaumu Serikali yao.
Akizungumzia hali ya utengenezaji barabara za vijijini, Mkuu
wa Wilaya ya Kilolo, mkoani humo, Gerald Guninita, alisema Wahandisi hutoa tenda kindugu zaidi bila kufuata taratibu.
Alisema hali hiyo inasababisha miradi mingi itekelezwe chini ya kiwango na kusisitiza ufike wakati kuwe na timu ya Mkoa ambayo itakuwa na jukumu la kukagua barabara zote zilizotengewa fedha kabla na baada ya matengenezo ili kuwathibiti makandarasi.
“Serikali inatoa pesa nyingi kuboresha barabara za vijijini, wapo Wahandisi na makandarasi ambao kazi yao ni kutafuna fedha wakishirikiana na watendaji wa halmashauri.
“Watendaji hawa hutoa tenda bila kuangalia uwezo wa mkandarasi, tumechoshwa na tabia ya ufujaji wa fedha, pia kuna tatizo kubwa la usimamizi wa barabara zetu, ufike wakati tuwe na uchungu wa fedha za Serikali na kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment