13 December 2012
JK: Temeke tengeni fedha kuboresha huduma katika hospitali, zahanati
Na Andrew Ignas
UONGOZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, umeagizwa kuhakikisha unatenga fedha za kutosha ili kuoboresha huduma na miundombinu ya Hosptali ya Temeke na zahanati zilizopo wilayani humo.
Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo hilo juzi wakiti akizindua
majengo ya huduma za mama na watoto yaliyopo katika Hospitali
ya Mbagala Rangi Tatu, iliyopo Zakhem, wilayani humo ambayo yamejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini.
Akizungumza na watendaji wa halmashauri hiyo, Rais Kiwete alisema manispaa hiyo inapaswa kuhakikisha katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/14, watenge fedha za kutosha ili
kuboresha huduma za matibabu na miundombinu.
“Hakikisheni mnatenga bajeti ya kutosha ili muongeze zahanati pamoja na vituo vya afya,” alisema Rais Kikwete na kuongeza
kuwa, Serikali ipo katika mazungumzo na nchi ya Korea Kusini
ili kupata mkopo wa dola za Marekani milioni 60,000 ili ziweze kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Mlunganzilwa.
“Serikali tayari imekamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Madaktari mkoani Dodoma, ambacho kinachukua wanafunzi 5,000, tupo katika mipango ya kujenga Hospitali ya Mluganzila ili madaktari hawa waweze kufanyia mafunzo yao hapo,” alisema.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dkt. Seif Rashid, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inatekeleza sera yake ya kujenga zahanati katika kata zote na vituo vya afya kwenye kila kijiji.
Mganga Mkuu wa manispaa hiyo, Dkt. Cylivia Mamkwe, alisema hadi sasa katika Wilaya hiyo kuna zahanati 35, vituo vya afya
viwili na hospitali tatu.
“Naipongeza Serikali kwa kuboresha huduma za afya tangu mwaka 2005, tulikuwa na zahanati 18 lakini hivi sasa zimeongezeka,” alisema Dkt. Mamkwe.
Alisema Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu imeborsha huduma za afya ambapo hivi sasa inahudumia zaidi ya wagonjwa 1,000 kwa
siku ambapo awali ilikuwa wagonjwa 350 kwa siku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment