13 December 2012

CCM, CHADEMA waungana kupigania haki za wanawake



Na Heckton Chuwa, Moshi

UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa asasi za
kiraia zaidi ya 30 zilizoshirikiana kuanzisha mtandao wenye
lengo la kushughulikia mambo muhimu yanayowahusu
wanawake katika Mkoa huo.


Mwenyekiti wa mtandao huo, Bi. Elizabeth Minde, aliyasema
hayo mjini Moshi juzi katika hafla ya kutia saini makubaliano
ya uundwaji wa mtandao huo.

Alisema lengo la makubaliano hayo ni kuziweka asasi hizo pamoja na kuhakikisha wanawake mkoani humo hasa waliopo vijijini wanaelimishwa na kutoa maoni yao kwenye tume inayoratibu mchakato wa Katiba Mpya.

“Hatua hii imetokana na taasisi inayohusika na masuala ya Haki
za Binadamu na Jinsia mkaoni hapa (KWIECO), kujumuisha
mambo ya wanawake na ushiriki wao katika mpango mkakati
wa 2012/16 kuhakikisha masuala ya wanawake yanapewa
kipaumbele katika uundwaji wa Katiba Mpya,” alisema.

Bi. Minde ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa KWIECO, alisema mtandao huo umeridhia kuandaa mpango kazi ambao pamoja na mambo mengine utaweka taswira bora ili kufanikisha
malengo yao ifikapo mwaka 2014.

“Kukosekana kwa mawazo ya kutosha ya wanawake katika michakato ya katiba zilizopita, kumechangia kuwepo kwa
mfumo dume kwenye jamii ambao umewafanya wanawake waendelee kuogelea kwenye madimbwi ya umaskini
ikilinganishwa na wanaume,” alisema.

Aliongeza kuwa, mtandao huo unatarajiwa kufanya mikutano ya kuhamasisha na kuwajengea uwezo wananchi ili kupanua uelewa wao juu ya mchakato wa Katiba Mpya wakitarajia kuwafikia watu 300,000 mkoani humo ambao watakuwa chachu ya wengine.

Alizitaja baadhi ya asasi zingine zinazounda mtandao huo kuwa ni Kiwakkuki, Nafgem, Ajiso, Tusonge CDO, Tawref, YWCA, KASI, Medicos Delmundo, Maua Women centre, Angaza women centre, Amani chidren centre, Wanawake Wakatoliki Tanzania, Idara ya Wanawake ya KKKT na Idara ya Wanawake ya BAKWATA.

No comments:

Post a Comment