13 December 2012
Rais Kikwete awatoa hofu Watanzania
Na Mariam Mziwanda
RAIS Jakaya Kikwete, amesema kupandishwaji hadhi kwa hospitali nchini na kuwa za rufaa, haufanyiki kwa vigezo vya maneno bali kinachoangaliwa ni ubora wa huduma bora na tiba za uhakika.
Alisema Serikali itaendeleza jitihada za kuboresha huduma
pamoja na na kuongeza wataalamu nchini.
Rais Kikwete aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua majengo ya hospitali katika vituo vitatu kikiwemo cha Mnazi Mmoja, Sinza na Mbagaka Rangi Tatu.
Alisema lengo la Serikali ni kuona wananchi wake wanapata huduma za uhakika karibu na maeneo waliyopo na kuondokana na ulazima wa wagonjwa kupelekwa Muhimbili kutokana na hospitali nyingine kutokuwa na uwezo.
“Kutokana na Serikali kutambua umuhimu wa sera ya afya nchini, tumeadhimia kuzipa kipaumbele hospitali zenye vigezo na sifa kuwa hospitali za rufaa kama ilivyo kwa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo na CCBRT, ambapo huduma zake zitakidhi matarajio ya huduma bora nchini,” alisema.
Alieleza mikakati ya utekelezaji wa sera ya afya inakwenda sambamba na upanuzi wa wigo katika taaluma ili kuongeza madaktari nchini na kuondoa tatizo la uhaba wa wauguzi katika hospitali za Serikali na binafsi.
Alisema utekelezaji wa mpango huo umezingatia uwepo wa ujenzi wa Hospitali ya Kisasa ya Rufaa ya Ruganzira katika manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam ambayo itatoa huduma sawa na Muhimbili hadi kufikia mwaka 2015.
“Matarajio ya Serikali mpaka kufikia 2015 Hospitali ya Ruganzira itaanza kutoa huduma, tena itakua ya kisasa yenye vifaa na huduma zote kutokana na kuwa ni hospitali ya rufaa itakayoshindana na Muhimbili, lengo ni kuona uwezo wa utoajia wa huduma unakamilika na wananchi wananufaika na huduam za afya nchini,” alisema.
Alisema hospitali hiyo pia itakuwa ikitoa mafunzo kwa wataalamu wa afya wa vyuo mbalimbali huku ujenzi wa hospitali ya ubongo na mishipa ya fahamu na ule wa hospitali ya huduma za figo mjini Dodoma ikiwa ni chachu ya maendeleo ya afya nchini.
Akizungumzia changamoto kubwa za afya katika Mkoa wa Dar es Salaam, alisema hospitali binafsi zinatakiwa kuhakikisha zinawekeza upande wa wataalmu, vifaa na tiba ili kuwa na ubora utakaopunguza msongamano wa watu.
Aliwataka watendaji wa hospitali hizo ambazo zimezinduliwa kuhakikisha zinatoa huduma bora ili kufikia malengo ya mileniam ya kupunguza vifo vya mama na mtoto. Naye balozi wa Korea Kusini, Chung Il, alisifu juhudi za Rais Kikwete kuhakikisha anaanzisha na kusimamia ujenzi huo kwa kutambua umuhimu wa malengo manne ya mileniam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment