03 December 2012
Ongezeko la watu tishio kwa huduma za jamii
Na Rachel Balama
ONGEZEKO la watu linaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye kasi kubwa ya kuzaliana duniani na kushindwa kikidhi huduma za jamii.
Kutokana na kasi hiyo, jitihada thabiti zinahitajika kudhibiti hali hiyo kutokana na ukweli kwamba rasilimali na ukubwa wa nchi ni vitu visivyoongezeka na kuweza kukabiliana na umaskini wa watu wake.
Ongezeko la watu linapaswa kwenda sambamba na kasi ya maendeleo, ikiwamo mipango miji. Ili hatua hiyo ifanikiwe, ndiyo maana serikali imeweka taratibu za kuhesabu watu wake ili iwe na kumbukumbu zinazohitajika.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na UNICEF kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi mwaka 2012 kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali wenye lengo la kujua hali ya ukuaji wa miji Tanzania na athari zake kwa watoto hasa wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi.
Mambo yaliyojitokeza katika utafiti huo ni kwamba miji ya Tanzania inakuwa kwa kasi, lakini hakuna usawa katika mgawanyo wa rasilimali na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii.
Hivi sasa takribani nusu ya idadi ya wakazi wa mijini nchini ni watoto ambapo mamilioni ya watoto katika miji wanakulia katika mazingira duni, njaa na manyanyaso ya kijinsia.
Pamoja na kwamba huduma nyingi zinapatikana zaidi mijini, wakazi wa maeneo yasiyo rasmi wanashindwa kuzipata kwa sababu mbalimbali ikiwemo umbali, gharama na vikwazo vingine.
Hali ya kimaisha ya wakazi waishio mijini inatisha na ni asilimia 16 tu ya watanzania waishio mijini ambao wana kipato cha kuaminika.
Maeneo mengi ya kuishi yanamilikiwa isivyo rasmi kwa sababu ya sheria ngumu zinazosimamia matumizi ya ardhi kwa hiyo nyumba hazina huduma muhimu na wakazi wa maeneo hayo hawako tayari kuwekeza katika kuyaboresha nyumba hizo.
Ni asilimia 20 tu ya nyumba katika makazi yasiyo rasmi ambazo zimeunganisha maji ya bomba, ujenzi holela wa makazi yasiyo rasmi kumezuia uchukuzi wa aina zote, pamoja na magari ya kuzoa taka, hali iliyosababisha takataka kulundikana.
Kwa muda mrefu kumekuwa na dhana ya kuwa watoto wanaoishi mijini wana maisha bora, ikilinganishwa na wale wa vijijini, lakini kwa Tanzania ubora wa maisha ya mijini unazidi kupungua.
Kwa mujibu wa ripoti ya miji na watoto hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa na serikali za mitaa kuanza kushughulikia matatizo ya maskini wanaoishi mijini pamoja na watoto wao.
Hiyo itawezesha kufuatialia kwa karibu hali ya umaskini, njaa na ukosefu wa lishe bora miongoni mwa jamii maskini zinazoishi mijini na kuweza kurahisisha upatikanaji wa suluhisho mbalimbali.
Hatua nyinginezo zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kuboresha hali ya maisha kwa kuimarisha mipango na usimamizi wa maeneo ambayo hayajapimwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kama maji, usafi wa mazingira na kuzuia ujenzi wa makazi katika maeneo hatari yanayokubwa na mafuriko.
Kushughulikia masuala ya umaskini na njaa kwa kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia kupata chakula chenye lishe bora na kuwaelimisha akina mama jinsi ya kutayarisha chakula chenye virutubisho na jinsi ya kulea na kuwalisha watoto.
Kujitayarisha kwa mabadiliko ya tabia nchi, serikali za mitaa zinaweza kusaidia jamii kuzuia majanga kwa kuchukua hatua ya kuboresha usafi wa mazingira na kutekeleza sheria zinazosimamia uzoaji wa taka na zinazozuia ujenzi holela.
Kuongeza upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira kwa kuwekeza zaidi katika huduma za maji na usafi wa mazingira pamoja na usafi kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inapatikana kadri ya mahitaji yake.
Kuboresha afya ya mtoto na kupambana na VVU na UKIMWI kwa kusaidia utafiti kuhusu vikwazo vinavyozuia familia maskini za mjini kupata huduma za afya, kama vile udhaifu katika mfumo wa msamaha wa kulipia gharama za matibabu, bima ya afya na uhaba wa huduma za afya za gharama nafuu na yenye uhakika katika jamii zenye kipato cha chini.
Kufikia elimu bora kwa wote kwa kuwasambaza walimu kwa uwiano sawa katika shule zote za mijini, walimu wawajibike kwa kuhudhuria shule na kuingia madarasani kila siku ya kazi na watoe mafunzo bora.
Utendaji wa walimu ufuatiliwe kwa kufuata viwango vilivyowekwa na katika kufuatilia utendaji wa walimu ni budi kushirikisha mamlaka za shule na wajumbe wa bodi za shule.
Kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na unyonyaji, sheria mpya ya watoto inazipa serikali za mitaa jukumu la kuhakikisha kuwa inawapatia watoto huduma muhimu za kijamii zinazozingatia kazi za watoto, mamlaka za serikali za mitaa zinaweza kufanya hivyo kwa kutekeleza sheria ndogo na kanuni pamoja na kukuza mipango ya kuwatunza na kuwalinda watoto.
Kuimarisha ushiriki wa watoto katika utawala kwa kufanya kampeni katika miji na ngazi za jumuiya zinaweza kuongeza ufahamu miongoni mwa wazazi, walimu, polisi mahakama na mamlaka za serikali za mitaa kuhusu umuhimu wa kuwawezesha na kuwasaidia vijana kushiriki katika shughuli za familia, shule na serikali za mitaa na manispaa.
Kwa mfano maeneo ya vingunguti kutokana na ujenzi wa nyumba holela kunapelekea kutokuwa na miundombinu ya maji safi na maji taka, hakuna sehemu za kutupa taka, hakuna maeneo ya kuchezea watoto jambo linalopelekea wakazi wa maeneo hayo kuishi ili mradi nao waishi.
Hali hiyo inaweza kusababisha athari nyingi kwa wakazi, wanafunzi na hata watoto wadogo kutokana na kuishi kwenye mazingira yasiyo na hadhi ya kuishi binadamu.
Kwa upande wa wanafunzi Asma na Mwajuma, wanasema wanaishi katika mazingira magumu kutokana na kutopata mahitaji muhimu kutokana na kipato duni cha wazazi wao.
Wanasema kutokana na hali hiyo wapo hatarini kupata mimba za utotoni na hata UKIMWI kutokana na kuwepo kwa vijana wengi ambao hawana shughuli hivyo wanaweza kuwarubuni.
"Huku muingiliano wa watu ni mkubwa na mbaya zaidi kuna watu wa kila aina hata walevi na wavuta bangi wapo hivyo ni rahisi vijana wa kike kurubuniwa na kuingia kwenye makundi maovu na hatimaye kukatisha masomo," anasema Asma.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya vingunguti, Protas Tarimo, anasema kuwa kukua kwa miji kunaathiri maendeleo kutokana na eneo kuwa na msongamano wa watu jambo linalochangia huduma za jamii kuonekana kama hazipo.
Anasema watoto wengi wanaishi katika maeneo hayo yamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na yenye vishawishi vingi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment