03 December 2012

Mimba za utotoni dodandugu linafuta ndoto za wanafunzi


UKATILI kwa wanawake na wasichana ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwakua unarudisha nyuma jitihada za kuwapa uhuru wa kufanya shughuli za maendeleo.


Utafiti wa Kitaifa  wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa zaidi ya  asilimia 39 ya wanawake hapa nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili  tangu wakiwa na umri wa miaka 15 na kwamba wengi wanafanyiwa  ukatili na wanaume waume zao ambao  ndio wana jukumu kulinda usalama na maslahi ya  wanawake, wasichana na watoto.  

Hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa katika ngazi ya Kimataifa, Kikanda na kitaifa ili kukomesha unyama huo unaorudisha nyuma maendeleo ya wanawake.

Hatua hizo ni pamoja na kuwepo kwa mikataba, maazimio na itifaki mbalimbali za kimataifa zinazohusu haki za binadamu na kupiga vita ukatili wa kijinsia.

Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kuondoa Aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake, (CEDAW 1979), Azimio na Ulingo wa Beijing, (1995) Maazimio  namba 1325, 1820, 1888 na 1889 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (2000) Azimio la kuleta Usawa wa Kijinsia katika Nchi za Afrika, (2004).


Pia, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu za Wanawake, (2006), Itifaki ya Maendeleo ya Jinsia ya Nchi za Kusini mwa Afrika, (SADC, 2008), na Malengo ya Milenia.

Aidha, Umoja wa Mataifa umekuwa ukifuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikataba hiyo kwa kuzitaka nchi husika kuandaa taarifa za utekelezaji na mafaniko yaliyofikwa.

Pamoja na kuwa baadhi ya nchi zimesaini na kuridhia mikataba hiyo, bado tatizo la ukatili kwa wanawake na wasichana linazidi kuongezeka.

Hivyo juhudi za ziada zinahitajika ili kuzuia na kutokomeza tatizo hili katika jamii zetu. 

Halikadhalika nchi husika zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali kwa lengo la kukabiliana na hali hii. Hatua hizo ni pamoja na kurekebisha Katiba za nchi husika ili zizingatie masuala ya jinsia.

Kuwepo kwa sera mikakati, mipango inayozingatia masuala ya kijinsia, kutunga sheria mpya zinazozingatia masuala ya usawa wa kijinsia na kurekebisha sheria kandamizi ili kuhakikisha kuwa wanawake wanapatiwa haki zao za kibinadamu.

Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, (AU), Umoja wa Nchi za kusini mwa Afrika (SADC) na Mwanachama wa Nchi za Maziwa Makuu,  imesaini na kuridhia mikataba Mikataba hiyo ambayo imezielekeza Nchi wanachama kuweka mifumo ya Kikatiba, Kisera na Kisheria kwa ajili ya kutokomeza tatizo la ukatili wa kijinsia.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Utafiti uliofanywa  na TAMWA mwanzoni mwa mwaka huu ulibaini kuwa tatizo hilo limeendelea kupoteza mwanga wa watoto wa kike, kwani wengi wao hukatisha masomo kwa kupata ujauzito.

Mfano halisi ni katika Mkoa wa Mtwara ambapo mwaka 2011 wanafunzi 214 katika Wilaya sita za Mkoa huo walikatisha masomo yao kutokana na mimba. Kati yao wanafunzi wa shule ya msingi walikuwa 66 na sekondari 148.

Wanafunzi wamekuwa wakikatisha masomo baada ya kupata ujauzito na kushindwa kuendelea na masomo huku familia zikibaki njiapanda kwa kukosa mtaalamu ambaye angewaongoza katika maisha.

Chanzo cha ubakaji ni tamaa za mwili za wanaume, hali hii hufanywa hata ni vijana wasio na shughuli maalumu pia watu wasio na huruma kwa watoto hao.

Mmoja wa mtoto aliyepata mkasa huo, jina tunalo mwenye umri wa miaka (14) akizungumza na mwandishi wa makala hii huku akiwa na mtoto wake wa miezi miwili anasema, alikuwa  darasa la sita katika Shule ya Msingi ya Chitekete mwaka 2011 mwezi wa tano akiwa anatoka shule alivamiwa na kijana aliyemtaja kwa jina moja la Hamadi (18) na kumbaka katika kichaka cha kuelekea nyumbani kwao.

Anasema, baada ya kufanyiwa unyama huo hakumweleza mzazi wake kwa kuhofia kupigwa na kijana yule, kijana huyo alikimbilia masasi huku mtoto akiendelea na masomo yake na kufanikiwa kujiunga darasa la saba mwaka 2012.

Binti aliendelea kuficha siri  hiyo hadi alipogundulika na mzazi wake January mwaka 2012 ambapo alikuwa amekaribia muda wake wa kufifungua, baada ya kuliona hilo alipata pia taarifa toka kwa Mkuu wa shule kuwa walimgundua mtoto wake kuwa ni mjamzito na hivyo hawezi kumaliza elimu ya msingi.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa ndoto ya binti huyo ambaye alitaka kuwa mwalimu hapo baada ya kuhitimu elimu yake ya juu.

Anaishi maisha ya taabu kutokana na kukosa uelewa wa kumtunza mtoto mdogo ambapo hushindwa kumpatia mahitaji muhimu.

"Siku nyingine nakosa hela ya kununua sukari, sijui mwisho wa maisha haya utakua lini," anasimulia huku akilia.

Baba Mzazi wa mtoto huyo (jina tunalo) amethibitisha kubwakwa kwa mtoto wake na kuwa kesi hiyo inaendelea na ana walakini kuwa haiwezi kuendelea kutokana na muendelezo wake.

Anasema mara ya mwisho ilitajwa Aprili 6 ambapo alijibiwa na mwendesha mashtaka kuwa, kesi hiyo ni ya kubaka na kusababisha mimba na inahitaji muda kusikilizwa na kuelezwa kuwa hawatakiwi kufika mahakamani hapo hadi watakapitwa kutoa ushahidi.

Mtendaji wa kijiji cha Chitekete, kata ya Chitekete, Shaibu  Hatibu ameoneshwa kukerwa na tukio hilo na kuahidi kukomesha matukio hayo ili kuwasaidia wanafunzi kujikwamua kiuchumi kupitia elimu wanayopata.

Sheria  ya elimu ya mwaka 1978 inayomtaka mwanafunzi anayebainika kuwa mjamzito kufukuzwa shule ni moja ya chanzo cha kushamiri kwa matukio ya mimba kwa kuwa haiwabani wapachika mimba.

Ni wakati muafaka sasa kwa serikali kuliangalia upya suala hili ikiwezekana kuzifuta sheria zilizopita na wakati ili kuwanusuru watoto ambao ni Taifa la kesho.

Kila mtu katika jamii atambue wajibu wake katika kuwalinda na kuwajengea mazingira rafiki ya kumaliza masomo kwa kuwaepusha na vishawishi, na wenye tabia ya kuwavamia watakoma tu wanafunzi hao wakiishi katika bweni.

Kitendo cha jamii kuendelea kuwaficha wahusika wa vitendo hivyo kunarudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau wa elimu zinazolenga kuboresha elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa kike nchini.

Serikali inatakiwa kuangalia uwezekano wa kuifanyia  marekebisho sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu wasichana wenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa idhini ya wazazi.

Hii pia inasababisha watoto wengi kukatisha masomo kwa kisingizio kuwa ni watu wazima.

Pia, taasisi na mashirika yanayotetea hali ya mtoto wa kike nchini yaungwe mkono ili kukomesha unyama huo na kulinda haki  ya mtoto kuozeshwa kwa lazima.


No comments:

Post a Comment