13 December 2012

Muswada sheria ya wananchi kupata taarifa kutua bungeni



Na Agnes Mwaijega

SERIKALI inatarajia kupeleka Muswada wa Sheria wa Haki na Uhuru wa Wananchi kupata taarifa zote muhimu kwenye taasisi
zote za Serikali katika kikao cha Bunge mwakani.


Waziri wa Katiba na Sheria Bw. Mathias Chikawe, aliyasema
hayo Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa shindano la uwazi ambalo liliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Twaweza
kwa kushirikiana na Serikali ili kupata maoni kutoka kwa
wananchi hasa vijana walio shuleni.

Alisema lengo la Serikali kupeleka muswada huo bungeni ni kuwezesha utungwaji wa sheria ambazo zitasimamia ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi, kuongeza uwazi na uwajibikaji wa Serikali kwa kushirikiana na wananchi.

“Mwakani tunapeleka muswada huu bungeni ili uweze kujadiliwa, lengo ni kuhakikisha Serikali inakuwa na ushirikiano wa karibu na wananchi,” alisema Bw. Chikawe.

Akizungumzia kuhusu shindano hilo, Bw. Chikawe alisema limelenga kuboresha sekta ya afya, maji na elimu ambapo kila mwananchi anapaswa kutoa maoni anayoona yanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta husika.

Aliongeza kuwa, shindano hilo litatoa nafasi kwa wananchi kushirikiana na Serikali kushughulikia changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hizo nchini kwa manufaa ya nchi.

Aliwataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao ili Mpango wa Kimataifa wa Kuendesha Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP), uweze kuwa na mafanikio kwa kutokomeza rushwa na kutumia teknolojia mpya ili kuimarisha utawala bora.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Twaweza, Bw. Rakesh Rajani, alisema wananchi watatoa maoni kuhusu namna ya kuboresha huduma za afya, elimu na maji ili kuleta mabadiliko.

“Vijana ambao ni wanafunzi, kama watatoa maoni bora katika shindano hili shule zao zitapewa kompyuta, ili kuongeza uwajibikaji  na uwazi nchini, upo umuhimu wa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuanzisha mfumo wa utoaji wa taarifa zote muhimu kwa wananchi,” alisema Bw. Rajani.

2 comments:

  1. YAKO MATAIFA YANAKERWA NA SHUGHULI ZA TWITTRE NA FACE BOOK MAONI YA WANANCHI MENGI HAYAJAPEVUKA INAPOFIKIA MWANANCHI ANASEMA KWANINI TUSISHIRIKISHWE KUACHANA NA ANALOJIA UNASHANGAA MBONA UTANDAWAZI MBONA HAMKUPIGA KURA HIVI UNAWEZA KUMZUIA NDEGE ASIRUKE JUU YA KICHWA CHAKO TANZANIA TUMEFILISIKA KIMAWAZO NI MUDA MUAFAKA TUWE NA MABUNGE MATATU KAMA ULAYA i.e HOUSE OF COMMONS,HOUSE OF SENATES ,HOUSE OF LORDS KWANI BUNGE LETU LINAPEWA MADARAKA MAKUBWA WAKATI HALINA UWEZO

    ReplyDelete
  2. Pongezi OMBENI SIFUE inaelekea siri za serikali sasa imekuwa vigumu kuzipata zilikuwa zinavuja sana wapinzani wanakosa mabomu ya kulipua magazeti nayo hayana jipya

    ReplyDelete