03 December 2012
Mbunge Wenje 'akalia kuti kavu' *Apewa siku 14 kuwaomba radhi Wamachinga
Na Daud Magesa, Mwanza
SHIRIKA la Umoja wa Machinga jijini Mwanza (SHIUMWA),
limemweka pabaya Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Bw. Ezekia Wenje, kwa kumpa siku 14 awe amewaomba radhi vinginevyo watamfikisha katika vyombo vya sheria.
Mwenyekiti wa shirika hilo, Bw. Ernest Masanja, alitoa tamko
hilo jana ambalo limesainiwa na viongozi wanne wa SHIUMWA kwa waandishi wa habari mjini hapa.
Shirika hilo linakanusha madai ya kuandika barua kwenda kwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, iliyodaiwa kusomwa na Bw. Wenje, katika mkutano wa hadhara ikidai shirika hilo linataka Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo Bw. Wilson Kabwe, aondolewe katika nafasi hiyo.
Bw. Wenye anadaiwa kuisoma barua hiyo Novemba 27 mwaka
huu, katika Uwanja wa Sahara na kudai kuwa, taarifa hiyo ambayo imeripotiwa katika vyombo vya habari imewafedhehesha sana.
“Kimsingi sisi tunakanusha taarifa hizi, hatujawahi kutoa tamko la aina hii kwa Waziri Mkuu Pinda au katika chombo chochote cha habari wala kwenye mamlaka yeyote ya Serikali.
“Tamko la Bw. Wenje limelenga kutuchonganisha kati ya shirika letu, Serikali na wamachinga wa jiji hili, tunalaani kitendo cha Bw. Wenje kutumia jukwaa la kisiasa kutoa taarifa ya uongo akitambua SHIUMWA si chama cha kisiasa,” alisema Bw. Masanja.
Alisema shirika hilo linaihakikishia Serikali ya jiji hilo kuwa haishiriki harakati zozote za kiasisa na haiko tayari kutumiwa
Aliongeza kuwa, SHIUMWA litaendelea kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria za nchi, utawala bora na katiba wakishirikiana na Serikali za Mitaa na Serikali Kuu.
“kutokana na hali hii, tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa Waziri Mkuu, Bw. Kabwe na wakazi wa jiji hili, taarifa hiyo ililenga kutuchonganisha sisi wamachinga na Serikali,” alisema.
Walimtaka Bw. Wenje awe muungwana kwa kuiomba radhi Serikali na SHIUMWA kutokana na kitendo chake cha kutoa taarifa zisizo za kweli katika mkutano wa hadhara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment