17 December 2012

Mashahidi wamkaanga Sheikhe Ponda



Na Rehema Mohamed

MKURUGENZI wa Kampuni ya Agritanza Ltd, Suleiman Mohamed (48), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Sheikh Issa Ponda na wenzake walivamia eneo la Chang'ombe Markaz kwa muda wa siku saba.

Mohamed ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo,alieleza hayo jana mbele ya Hakimu,Victoria Nongwa wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya uvamizi wa eneo hilo inayomkabili Sheikh Ponda na wenzake.

Huku akiongozwa na wakili wa Serikali, Tumaini Kweka,shahidi huyo alidai kuwa wakiwa katika eneo hilo walianza ujenzi wa jengo mfano wa banda wakitumia vifaa vya ujenzi vilivyowekwa na Kampuni ya Agritanza Ltd kwa ajili ya kujenga uzio.

Alidai kuwa walikwenda kujenga uzio katika eneo hilo baada ya kufikia makubaliano ya kubadilishana eneo hilo la heka 4 na heka 4 zilizopo Kisarawe baina yao na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA)

Hata hivyo alidai kuwa kabla ya kuanza ujenzi wa uzio huo,walipata taarifa kutoka kwa mlizi wao kuwa Sheikh Ponda hakupendezewa na kitendo cha kampuni hiyo kumiliki eneo hilo walilobadilishana na BAKWATA.

Alidai kuwa kutokana na kuwepo kwa tetezi hizo,aliwaamuru watu aliowapeleka kuanza kuchimba msingi wa kujenga uzio kusitisha kufanya hivyo, ili waweze kutafute muafaka wa suala hilo kwanza.

"Siku ya Ijumaa saa 10 jioni,nilipita eneo hilo nikakuta watu wengi kama 400 hivi,watu hao walikuwa wakizunguka eneo hilo,baadaye walipungua na walipoondoka vifaa vyetu vya ujenzi tulivyoviweka kama mchanga,kokoto na matofali vilipungua na vingine kutokuwepo kabisa,"alidai, Mohamed

Kwa upande wake Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sheikh Ismail Makusanya (49) aliieleza mahakama hiyo kuwa Baraza la Maulamaa liliidhia kubadilishana eneo la Chang'ombe Malkas kutokana na kuridhika kwa ukubwa wa eneo la Kisarawe walilopewa na Kampuni ya Agritanza Ltd.

Alidai kuwa akiwa kama mmoja wa wajumbe wa baraza la Maulamaa,alikuwa miongoni mwa wajumbe waliokwenda kukagua eneo hilo la Kisarawe na kuridhika nalo.

Alidai kuwa eneo la Chang'ombe Markas ni halali kwa Kampuni ya Agritanza kwa kuwa walifuata taratibu zote za kubadilishana eneo hilo ikiwa ni pamoja na kusaini mkataba wa makubaliano baina yao na Bakwata.

Katika kesi hiyo Sheikh Ponda na wenzake wanadaiwa  kuvamia eneo la Markaz, Chang'ombe jijini Dar es Salaam, ambapo waliharibu  na kuiba mali mbalimbali zenye  thamani ya shilingi milioni 59.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 18 mwaka huu.

1 comment:

  1. Bakwata eleweni kesho mbele ya Mwenyezi Mungu mutakuwa masuuli kutokana na munayo yafanya dhidi ya sheikh Ponda.
    Kwani sasa munazidi kutupa wasiwasi juu ya madhumuni ya chombo hicho ambacho tulidhani kitakuwa na maslahi kwa Waislamu lakini kinyume chake kimekuwa kikandamizaji kwa Waislamu.
    Duniani ni mapito tu hivyo mujuwe kwamba ipo siku mutarejea kwa Alla Subhanahuu Wataaala na hapo ndipo mutakapo jibu dhidi ya maovu yenu yote mnayo yafanya dhidi ya Waislamu wenzenu.
    Bakwata malengo yake yote sasa yamepotea imekuwa ni baraza kuu la walaji tanzania hivyo bakwata sasa ndio msimamizi mkuu wa kurudisha nyuma Uislamu na Waislamu katika nchi hii. Mimi nawakumbusha kuvimba kwenu matumbo kwa sababu ya ulaji isiwe sababu ya kuwadhalilisha Waislamu.

    ReplyDelete