17 December 2012
CHADEMA yambwaga Bulembo kortini
Na Rehema Mohamed
MWENYEKITI wa Taifa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,Abdalah Bulembo, ameangukia pua baada ya Mahakama ya Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kumvua udiwani, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kijitonyama kwa tiketi ya CHADEMA, Uloleulole Athumani.
Uamuzi huo ulitolewa jana Jaji Upendo Msuya, aliyekuwa akisikiliza rufaa iliyokatwa na Athumani ambapo aliridhika na hoja za mrufani (Athumani) za kupinga hukumu iliyomvua wadhifa huo.
Katika hukumu hiyo, Jaji Msuya alisema kwamba Athumani alishinda kihalali na kwamba hakuna sababu za msingi za Mahakama ya Kisutu kumvua wadhifa huo.
Kutokana na uamuzi huo,mahakama hiyo imemrejeshea Athumani wadhifa wake wa udiwani wa Kata ya Kijitonyama, kupitia CHADEMA.
Awali Athumani alitangazwa kuwa diwani wa kata hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, baada ya kumshinda mpinzani wake wa karibu, Abdallah Bulembo wa CCM.
Baadaye Athumani alivuliwa wadhifa huo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutokana na aliyekuwa mgombea wa wadhifa huo kupitia CCM (Bulembo) kufungua kesi katika mahakama hiyo akipinga ushindi wake.
Athumani alikata rufaa Mahakama Kuu Dar es Salaam, akipinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu na jana aliibuka kidedea baada ya mahakama hiyo kumrejeshea wadhifa wake huo.
Katika kesi ya msingi, Bulembo alitoa sababu sita za kutokuridhishwa na matokeo hayo ambapo miongoni mwa sababu hizo za kupinga matokeo hayo ni pamoja na tofauti ya majina yake katika nyaraka mbalimbali zilizohusiana na uchaguzi huo.
Aliiomba mahakama hiyo itengue matokeo hayo yaliyompa ushindi mdaiwa kwa kutamka kuwa yalikuwa ni batili na badala yake imtangaze yeye kuwa ndiye mshindi.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Genvitus Dudu, ilikubaliana na madai ya mlalalmikaji na kutengua matekeo yaliyompa ushindi Athumani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment