27 December 2012

CHADEMA wajibu hoja ya CCM *Ni kuhusu ubunge wa Lema na utawala bora



Na Goodluck Hongo

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinapaswa kuwaeleza Watanzania ukweli wa mabilioni yaliyofichwa nje ya nchi na hatua iliyochukua badala ya kujifanya wasemaji wa Ikulu na Serikali.


Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na gazeti hili ili kujibu mapigo
ya CCM kuwa, ushindi wa rufaa ya Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema ni matokeo ya utawala bora wa Serikali ya chama tawala.

Alisema chama chao kiliwahi kuilalamikia Ikulu juu ya kuingilia kesi ya kesi ya Bw. Lema lakini wanaojibu ni CCM.

Aliwataka Watanzania wakumbuke kuwa, CCM kupitia makada wake ndio waliofungua kesi kupinga matakwa ya wananchi wa Arusha Mjini ambao walimchagua Bw. Lema kuwa mbunge
wao na kuhoji utawala bora uko wapi kwa chama tawala.

“Kama CHADEMA isingekata rufaa, kuwa na mawakili makini au kukosa uwezo wa kutetea haki ya wananchi kuhusu maamuzi ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, leo hii Bw. Lema asingekuwa mbunge wa jimbo hilo,” alisema Bw. Mnyika.


Aliongeza kuwa, ni vyema CCM ikaacha propaganda badala yake kabla ya kwenda mikoani, wawaeleze wananchi hadi sasa vigogo wangapi wamejivua gamba, wamewaondoa mafisadi wangapi serikalini na kuwafilisi mali zao.

“Pesa za walipa kodi zilizofichwa nje ya nchi na sio Uswisi pekee bali hata katika visiwa vya Mauritius, kama kweli CCM inataka kumrdia Mungu itekeleze haya kwanza,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa katiba, Serikali inawajibika kwa wananchi ambao ndio wenye madaraka na mamlaka yote hivyo Serikali inapaswa kuwajibika kwa wananchi badala ya CCM.

Aliitaka CCM kuisoma kwa makini Katiba ya Chadema, ibara
ya tatu kuhusu nguvu ya umma ndio maana Kamati Kuu ya CHADEMA iliazimia mwaka 2013 ni wa kuishinikiza Serikali kuwajibika kwa wananchi kupitia nguvu ya umma si vinginevyo.

“Kitendo cha CCM kutangaza kuwa mwaka 2013 ni wa kazi ina maana siku zote walikuwa wamekaa badala ya kuwajibika kwa wananchi tangu washike madaraka,” alisema Bw. Mnyika.

1 comment:

  1. KUJIVUA GAMBA NINI AU UFISADI NI NINI MBONA WABUNGE WANAISHI MAISHA YA KIFAHARI WANANCHI WA KAWAIDA WAKITESEKA WAKIWA BUNGENI KAZINI KUPELEKA HOJA BINAFSI ILI KUVURUGA RATIBA YA BUNGE WAONGEZEWE MUDA WA KUPATA POSHO WAKIWA DODOMA NI KUTANUA NA MACHANGUDOA BILA KUFIKIRIA WANAENEZA UKIMWI WAKATI MWINGINE MTU UMAFIKIRI MBUNGE NI WA NINI KWANI YOTE MUNAYOZUNGUMZA BUNGENI HATUKUWATUMA NI LINI KABLA YA VIKAO VYA BUNGE MULIZUNGUMZA NA WAPIGA KURA WENU????

    ReplyDelete