03 December 2012
Lowassa: Makanisa yawasaidie vijana nchini wapate mashamba
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa, ameyataka makanisa nchini kuwasaidia vijana kupata mashamba ili wakabiliane na tatizo la ajira.
Bw. Lowassa aliyasema hayo katika sherehe za uzinduzi wa DVD
na harambee ya ununuzi wa basi la kwaya ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Msasani, Dar es Salaam.
Alisema kufanya hivyo, makanisa yatakuwa yamesaidia juhuzi za Serikali kukabiliana na tatizo kubwa la ajira kwa vijana nchini.
Alisema umefika wakati wa makanisa mbalimbali kushiriki katika harakati hizo kama yanavyofanya katika sekta ya elimu na afya.
“'Nayaomba makanisa yaliyopo nchini yasaidie kuwatafutia vijana mashamba ili waweze kujihusisha na kilimo, hii ni sekta ambayo kwa sasa inapewa msukumo mkubwa na Serikali kupitia mpango
wa Kilimo Kwanza.
“Kilimo kinaweza kuondoa tatizo la ajira hivyo ni jukumu letu kuwasaidia vijana waweze kujiingiza katika sekta hii, makanisa
ni taasisi zinazoweza kutoa msaada mkubwa wa kuwawezesha vijana kupata mashamba,”' alisema.
Kwa upande wake, Mchungaji wa usharika huo, Eliguard Muro, alimshukuru Bw. Lowassa kwa mchango wake mkubwa kwenye jamii na kushiriki katika harambee mbalimbali za kikanisa.
Katika harambee hiyo, zaidi ya sh. millioni 100 zilichangwa ambazo ni fedha taslimu na ahadi ambapo Bw. Lowassa ambaye aliongoza harambee hiyo alichangia sh. milioni 10 na wanawe wakitoa sh. milioni tano.
Malengo ya harambee hiyo yalikuwa kuchangisha sh. milioni 100 ambapo pamoja na mambo mengine, Bw. Lowassa amekuwa akitumia majukwaa katika shughuli mbalimbali anazoalikwa kuelezea ukubwa wa tatizo la ajira kwa vijana nchini
akilifananisha na bomu linalosubiri kulipuka.
Katika majukwaa hayo, Bw. Lowassa amekuwa akisisitiza kuwa, jukumu la kuwaokoa vijana na janga hilo ni la kila Mtanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Mungu akubariki Ndugu Edward Ngoyayi Lowasa. Mungu unayemtumikia hatakuangusha. Songa mbele na Mungu akufanikishe katika kazi njema unayomtumikia BWANA.
ReplyDelete