Na Danny Matiko
MMOJA wa wasanii maarufu nchini, Bw Hussein Ramadhan Mkieti, a.k.a 'Sharo Milionea', alifariki dunia mwanzoni mwa wiki hii kwa ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa Novemba 25, mwaka huu, ambapo gari aliyokuwa akiendesha safarini ilipoteza mwelekeo na kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea kwenye kijiji cha Songa-Kibao, Wilayani Muheza, Mkoa wa Tanga, wakati marehemu akitokea Jijini Dar es Salaam kwenda nyumbani kwao Lusanga, pia Muheza.
Taarifa zinaeleza kuwa marehemu Hussein Ramadhan Mkieti (27) alifariki popo hapo kwenye eneo la ajali, lakini pia licha ya kupoteza uhai wake, wananchi walimpora mali zake zote, ikiwemo kumvua mavazi yake yote, kupora simu na fedha zake zote ambazo mpaka wakati tunakamilisha Makala haya idadi yake haikuweza kufahamika kwa uhakika.
Kadhalika, mashuhuda katika eneo la ajali walikaririwa kueleza kuwa marehemu aliporwa mizigo yake yote ambayo inadhaniwa ni pamoja na zawadi alizokuwa anawapelekea ndugu zake, wakiwemo wazazi wake.
Kwa mujibu wa Mwandishi wetu aliyeshuhudia mazishi ya msanii huyo Novemba 29, 2012, kijijini Lusanga, serikali ilisema itawatafuta wote waliopora mali ya marehemu huyo na kuwafikisha mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake dhidi ya unyama wao.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Bi. Subira Mgalu, ambaye aliwataka waporaji wote kusalimisha mali ya marehemu kwa mamlaka husika katika eneo hilo au kwa ndugu wa marehemu.
Mkuu wa Wilaya alitoa tamko hilo la Serikali kutokana na vitendo vya wananchi wa eneo ilipotokea ajali hiyo kuamua kumpora marehemu Hussein mali zake zote, ikiwemo kumvua mavazi yake aliyokuwa amejisetiri nayo safarini.
Mkuu wa Wilaya alisema wote waliotenda ukatili huo wanafahamika, na kuongeza kuwa "jisalimisheni wenyewe pamoja na vitu mlivyopora kabla ya serikali kutumia nguvu za dola kuwasaka na kuwakamata wote mliohusika, kwani mnafahamika."
Wakati tukitafakari maafa yaliyoikumba familia ya marehemu huyo, ikiwemo kadhia ya uporwa mali zake ajalini, ni budi jamii ilaani vitendo vyote vya aina hiyo ambavyo vimeshamiri katika mikoa mingi nchini.
Ni dhana potofu, hususan katika kizazi hiki, kudhani kuwa utajiri humuijia mtu kwa kupora mali kwa dhuluma.
Kauli hiyo ya Serikali kwamba itatumia mkono wake mrefu wa kisheria kuwanasa watu walioiba vitu vya marehemu 'Sharo', imekuja kwa wakati wake, kwani waporaji wa mali za wahanga wa ajali huwa wanafahamika.
Ni mawazo potofu mno kudhani kuwa twaweza kuwa matajiri kwa kupora na kudhuru fiziki ya wengine, kwani kanuni ya utajiri inamtaka mtafuta utajiri huo kubuni mikakati ya kupata mali bila kuwadhuru wenzake kwa namna yoyote.
Kufanyakazi kwa bidii na kuwa na mikakati endelevu ya kubuni njia mbalimbali za kukuza hicho "kidogo" unachopata, ndio mbinu bora ya kuelekea kwenye utajiri ambao kila mmoja anauwania.
Matajiri wote, akiwemo maarufu kuliko wote, Bill Gates wa Marekani, walipata utajiri kwa kupitia mikakati chanya na ubunifu peke yake bila kumpora mtu mali zake, ikiwemo kuvunja majumba usiku wa manane.
Hebu angalia kwamba nyingi ya ajali za barabarani hutokea karibu na vijiji palipo na watoto, ambapo hao hushuhudia ukatili wa wakubwa kuwapora mali wale wanaopatwa na ajali.
Hiyo ina maana kuwa watoto nao hukua wakiwa na mtazamo kuwa ni kawaida kwa binadamu kuwapora majeruhi na marehemu wanaokumbwa na ajali, badala ya kuwasaidia kwa haraka.
Sasa kama watoto wanalelewa kwa mitindo ya namna hiyo, jamii yetu inaelekea wapi kama si katika ukatili mithili ya unyama,?
Inasikitisha na kuhuzunisha mno, na kwa kweli mtu anabaki kujiuliza maswali mengi bila majibu, na hasa ikizingatiwa kuwa waporaji huwa ni watu wanaofahamika katika maeneo ya ajali.
Laana ya kufanya mzaha na marehemu ni mbaya mno kuliko inavyodhaniwa, ambapo hiyo inatokana na kwamba marehemu huwa ni "mwili" ambao awali ulihifadhi roho ambayo sote twajua kuwa ni pumzi ya Mwenyeza Mungu.
"Pumzi" hiyo ambayo ni roho iliyo hai imefungamanishwa pamoja na mili hii ambayo huwa tunarithi kutoka kwa wazazi wetu, ambapo "pumzi" hiyo huweza kuondoka na kutoweka pale inapobaini kuwa mwili umepoteza uwezo wa kuendelea kufungamanishwa pamoja nayo.
Kuondoka kwa roho kutoka mwilini, tafsiri yake ni kifo, ambapo neno "kufa" limetokana na mwili kupata "ufa" ambao husababisha kuvuja kwa "pumzi" kutoka mwilini.
Mwili unapopata "ufa" huwa hauwezi kuendelea kuhimili kufungamanishwa na "pumzi" ambayo maana yake sahihi ni roho, na roho tafsiri yake ni "kiini cha uhai" ambao ni sehemu ya Mwenyezi Mungu.
Sasa basi kama tunaweza kukubaliana na mantiki katika aya hiyo kwamba roho ni kiini cha uhai wa binadamu, na pia kwamba roho ni sehemu ya Ukuu wa Mwenyezi Mungu, itakuwa sahihi kusema kwamba mwili wa binadamu kufungamanishwa na roho ya Mungu huufanya mwili huo kuwa sehemu mojawapo ya Mungu.
Hivyo basi, kuondoka kwa "pumzi" na kurejea katika himaya ya Mwenyezi Mungu na kuuacha mwili, si sababu ya kutusababisha binadamu tunaosalia kuwa hai kufanya mzaha na mwili huo kwa namna yoyote ile.
Hiyo ni pamoja na kutokuwa na ruksa ya kuupora mwili huo ambao unahitaji kupumzishwa kwa staha zote.
Inapotokea mtu kufariki, hata kama alikuwa ni aduio yako, ni vyema kuujali mwili wake na kuuhifadhi kwa lengo la kusubiri taratibu za kuuzika badala ya kuufanyia dhihaka kama ya kuuvua nguo zake.
Hiyo ikiwa na maana kwamba mzunguko wa kimaumbile hukamilika pale ambapo 'pumzi', yaani roho, hurejea juu kwenye himaya iliyo tofauti na hii ya kibinadamu, na 'mwili' hurejea chini ardhini; na hivyo, kukamilisha ulinganifu wa kimizani kwamba "ilivyo juu mbinguni na chini pia duniani."
Tukiwa sehemu katika jamii iliyoelimika hivi, tunapaswa kuwaonesha watoto na pia kuwafundisha mapema namna ya kuwa raia wema katika maisha yao ili waepuke uhalifu unaoweza kuwasababishia majanga mbalimbali ya kidunia.
Lakini, badala ya hayo, tunawaonesha jinsi ya kuwa wakatili, ikiwemo kupora mali za marehemu. Hiyo ni tabia mbaya kabisa na ya kinyama.
Wananchi mnaoishi kando ya barabara, na kwingineko, ikiwemo Wilaya ya Muheza, na Mkoa wa Tanga kwa ujumla, ni budi kuliona tukio la kupora mali za marehemu Hussein Ramadhan Mkieti, kama ni changamoto ambayo inaweza kuwa na athari mbaya kwa jamii na hivyo kulikemea kwa uzito unaostahili.
Baadhi ya Imani hufundisha kuwa "pumzi" ambayo imejiondoa kutoka kwenye mwili wa binadamu ambao umepoteza uwezo wa kuendelea kuihifadhi, hulia mbele ya Mwenyezi Mungu inapoona mwili ambao awali ulikuwa makazi yake, ukidhihakiwa na binadamu ambao wanachukuliwa kuwa viumbe wenye akili timamu kuliko wanyama, miti, mawe, na kadhalika.
Inaaminika kuwa athari yaweza kuwa mbaya zaidi kwa jamii husika kama Mwenyezi Mungu akiamua kuijibu "pumzi" hiyo katika namna ambayo ataona inafaa, ambapo pia kama majibu hayo yatakuwa hasi itakuwa ni laana mbaya.
Hivyo, ni vyema jamii kuhakikisha kuwa wahanga wote wa ajali ndogo na kubwa, wanasaidiwa kwa kuondolewa haraka kutoka katika eneo la ajali na kufikishwa katika sehemu ambayo watapatiwa msaada wa kitabibu, na pia hifadhi kwa marehemu.
Hiyo ni pamoja na kuepuka kupora mali zao, kama ilivyotokea Muheza, au sehemu nyinginezo.
No comments:
Post a Comment