24 December 2012
Jamii yashauriwa kushiriki mafunzo ya mgambo
Na Andrew Ignas
KAIMU Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam Bw.Raymond Mushi ameiasa jamii kuachana na imani potofu kuwa mafunzo yanayotolewa kwa mgambo ni sera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo hakuna umuhimu wa kupata mafunzo hayo.
Kauli hiyo imetolewa juzi Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya kozi ya mgambo ya awamu ya 51 mkoani humo yaliyofanyika katika viwanja vya Jeshi vya Mgulani.
Alisema kuna idadi kubwa ya watu wanaofikiri kuwa utolewaji wa mafunzo hayo ni kutekeleza sera ya CCM jambo ambalo halina ukweli wowote badala yake wanatakiwa kuwa mabalozi katika kuelimishana ili jamii itambue umuhimu wa kupata mafunzo hayo.
"Naomba ikumbukwe kuwa Tanzania baada ya uhuru Hayati Baba ya Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1970 aliamua kuanzisha mgambo kwa lengo la kuwaandaa vijana kiujuzi, "alisema Bw.Mushi.
Hata hivyo ameiomba serikali kuhakikisha anaanda bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuendesha mafunzo mbalimbali kwa mgambo ili kusaidia shughuli za kijamii ikiwemo majanga ya moto,mabomu na ulinzi shirikishi.
Alisema kuwa pia atahakikisha wanazungumza na makampuni ya ulinzi ili kuwapa vipaumbele vya ajira kwa wahitimu hao.
Naye mshauri wa mgambo mkoani humo Kanali James Sarungi alisema jumla ya wakufunzi 229 wamehitimu ambapo Ilala ni 139,Temeke 120 na Kinondoni 160.
"Tulianza mafunzo Agosti 13, mwaka huu tukiwa na washiriki 439 toka wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam hata hivyo kumalizika kwa wahitimu 229 kumetokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiuchumi,"alisema.
Alisema mpaka sasa sera hiyo ya ulinzi na usalama ambayo lengo kupata mgambo 300 kwa kila mwaka inashindwa kufikia kutokana na kubezwa kwa mafunzo hayo kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kazi ya walalahoi.
Naye mshauri wa migambo kutoka Wilaya ya Temeke Meja Begabena alisema kuwa atahakikisha anajipanga ipasavyo ili kutoa mafunzo hayo kwa ngazi yote ya serikali ya mtaa na kata.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment