24 December 2012
Tutaendelea kutegemea misaada toka Ulaya mpaka lini Watanzania?
Na Michael Sarungi
KATIKA nchi nyingi za kiafrika Tanzania ikiwa ni moja wapo imeshakuwa ni kama mila na desturi kwa kuendeleza kujiendesha kwa kiwango kikubwa kwa kutegemea misaada toka kwa wale wanaowaita wafadhili toka nje.
Lakini ukichunguza kiundani mara nyingi utagundua kuwa mingi ya misaada hiyo si chochote zaidi ya kuendelea kuwadidimiza kimaendeleo wananchi wa nchi husika.
Kwa mfano mojawapo ya malengo ya Benki ya Dunia kama taasisi ya kipesa iliyo chini ya mataifa makubwa ya kiulimwengu yenye viwanda ni kuhakikisha ukuaji wa biashara sawia kimataifa, lakini kiukweli huo ni unafiki tu kwani fedha za nchi hizi za kiafrika hazina nafasi kwenye soko la dunia.
Hebu angalia hata maligafi toka kwenye viinchi hivi vya kiafrika vinavyo nunuliwa kwa bei ya kupunjana katika masoko ya kimataifa na hakuna juhudi zozote za makusudi zinazo fanywa na wakubwa hao kukabiliana na janga hilo.
Wakati hali ikiwa ni hivyo kwa maligafi toka katika ukanda huu wa kiafrika mali toka huko ulaya zinapo kuja katika mabara haya ya kiafrika vinauzwa kwa bei ya gali kiasi cha mwananchi wa kawaida kushindwa hata kuuliza bei.
Mpaka kufikia hapo je kuna uwiano wa kibiashara katika ulimwengu huu sana sana katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia nchi hizi za kiafrika kugeuzwa kuwa ni sawa na madampo ya bidhaa feki toka ulaya na marekani.
Na sote tumekuwa ni mashahidi wa kujionea kila siku bidhaa feki vikiteketezwa na mamlaka husika pindi zinapo kuwa zimebainika, lakini ukweli ni kuwa hali inatisha katika ukanda huu wa kiafrika.
Hii ni dharau kwa nchi zetu hizi za kiafrika kwa sababu kama mtu anajua kuwa bidhaa hizi ni feki halafu anatumia umasikini wako kukuletea ni sawa na mtu kukuywesha sumu inayo ua taratibu.
Pamoja hali kuwa hivyo lakini bado tunaendelea kuwachekea hao wazungu toka ulaya na marekani kana kwamba ni watu walio wema maishani kwetu kumbe ni panya buku anaye kung’ata na kupulizia.
Kwa kudhihirisha kuwa hawa siyo watu wema hebu jaribu kuiangalia hata misaada mingi inayo tolewa na hawa tunao waita majina ya wafadhili kuja kwenye nchi hizi za dunia ya tatu, mingi inatolewa kwa mashariti magumu sana na mingi inageuka kuwa ni mizigo kwa nchi husika.
Mingi ya misaada hii ni ya kinafiki na ambayo haina nia njema kwa wakazi wa bara hili lakini cha kushangaza hata viongozi wengi wa mataifa haya ni kama wamefikia ukomo wao hata wa kufikiri.
Imefikia wakati hata bajeti nyingi toka katika viinchi hivi vya kiafrika kwa kiwango kikubwa vinategemea pesa toka huko Ulaya na Marekani wakubwa hao wasipo toa pesa hizo ni matatizo.
Nchi nyingi za kiafrika zimegeuka na kuwa sawa na motto mdogo anaye sumbuliwa na ugonjwa wa utapia mlo kiasi cha kushindwa kuweza kusimama mwenyewe kwa miguu yake bila ya misaada toka kwa watu wengine.
Afrika ni lazima ikomeshe hali hii ya kuendelea kunyonya maziwa haya ya sumu toka huko Ulaya na Marekani kama kweli inautaka uhai wake katika miaka mingi ijayo.
Ni ukweli usio weza kupingika kuwa mashariti yanayoambatana na misaada hii kwa kiwango kikubwa sana yanachangia kushusha thamani ya pesa zetu katika viinchi vingi vya kiafrika hii inaambata na hizi biashara huria zinazo endeshwa bila ya usimamizi wa serikali za nchi husika.
Hali hii kwa miaka ya hivi karibuni imesababisha afrika kuzidi kuzama na kuelekea kusiko julikana kiuchumi na hasa linapo kuja suala la biashara za kimataifa.
Mengi ya mashariti hayao kwa kiwango kingine yamekuja na madhara makubwa sana hata kwa ustawi wa wakazi wa bara hili kwa mfano wengi wanatoa mashariti kama kupunguza wafanya kazi na ubiafsishaji wa makampuni.
Wenzetu hawa toka ulaya siku zote ni watu wa kuangalia maslahi ya kwao na hata siku moja mzungu hawezi kuja hapa halafu utarajie kuwa ana malengo mazuri ya kukusaidia huo ni uongo.
Mataifa haya toka Marekani na Ulaya hata siku moja haya wezi kufurahia kuziona nchi hizi za kiafrika zikipiga hatua za kimaendeleo kwa sababu ya kukosa raslimali asili na maligafi kwa manufaa ya viwanda vyao.
Hebu ziangalie nchi hizi za kiafrika ni ipi inayo weza kusimama na kusema kuwa inafanya biashara inayoeleweka na nchi za ulaya au marekani zaidi ya kuendelea kukandamizwa kila kukicha.
Nchi zetu hizi za kiafrika Tanzania ikiwa ni mija wapo ni lazima zielewe kuwa kuendelea kuitegemea misaada hii toka Ulaya na Marekani ni kuendelea kuudhalilisha utu wetu.
Kwanini nchi kama Tanzania iendelee kuwa omba omba kila kukicha wakati tumejaliwa kuwa na kila kitu kuanzia madini ya kila aina, ardhi nzuri yenye rutuba, mbuga za wanyama zenye wanyama wa kila aina, mito, maziwa na raslimali nyingine nyingi?
Kwangu mimi huu ni udhaifu wa hali ya juu na ni aibu kwa wahusika walio kabidhiwa dhamana ya kuliongoza taifa hili kama baada ya zaidi ya miaka hamsini ya uhuru tuna letewa misaada ya vyandarua halafu wao wanaondoka na madini yetu ni aibu iliyoje hii?
Hii ni misaaada ambayo imekuwa ikipora uhuru wetu wa kuwa na maamuzi yetu wenyewe na ukiitazama kiukweli ni uvivu wa kufikiri tu ndio unao tusumbua waafrika wa leo mbona waasisi wetu wa mwanzo walifanikiwa kwa kiwango kikubwa japo hawakuwa wameanza kuzitumia raslimali kama ilivyo sasa?
Mingi ya misaada hii haina tofauti na nyama anayo pewa mgonjwa baada ya kun’olewa meno kama mashariti ya kupewa nyama hiyo huu ni upuuzi usio kubalika hata kidogo.
Waafrika na watanzania ni bora tukajua kuwa bila ya bara hili la afrika Ulaya na Marekani wasingeendelea na kufikia huko waliko nchi hizo zimepiga hatua kubwa kwa kutegemea raslimali toka afrika.
Raslimali walizozichuma toka afrika na nguvu kazi toka huku hususan wakati wa utumwa na uongozi wao wa kujali maslahi ya nchi zao ndivyo vilivyo wafikisha hapo walipo sasa.
Leo hii tunashuhudia nchi nyingi za kiafrika zikishindwa hata kupumua kwa sababu ya ukoloni mambo leo unao zidi kushika kasi kwa kusaidiwa na viongozi wenyewe wa kiafrika.
Hivi kuna haja ya nchi kuiita kuwa iko huru kama viongozi wake wanajipendekeza kwa kiongozi wa nchi iliyo endelea kuliko hata wananchi wake walio mchagua hapa kuna uhuru wa kweli?
Nchi kama Tanzania ya leo iliyo barikiwa na kila kitu kuendelea kukumbatia misaada toka huko ulaya na marekani ni kujihalisha kuwa ni dhaifu na goigoi mbele ya wenzetu walio endelea.
Hii ndiyo maana hata viongozi wetu wengi wamesahau hata majukumu yao na kuwa makuhadi wa ukoloni mambo leo, wamesahau kabisa kuwa wanapashwa kuonyesha njia kuelekea kwenye nchi ya ahadi walio iahidi kuwafikisha wananchi walipo kuwa wakiomba kura.
Afrika ni lazima sasa tuikatae misaada hii isiyo kuwa na tija kwetu waafrika wenyewe tusimame kwa kuitumia raslimali yetu wenyewe na kuacha ubinafsi wa wachache kujilimbikizia mali huku wengine wakilia njaa.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha viongozi wetu hawa kuwa udahaifu wao wa kuweza kuwa na misimamo ya kweli machoni mwa wakubwa hawa ni aibu kwao kwani ipo siku historia itawahukumu mbele ya safari tafakari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment