17 December 2012

Kesi ya washitakiwa wa Mbagala yaiva


Na Rehema Mohamed

UPANDE wa Mashtaka katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha na kuharibu mali zenye thamani ya sh.milioni 500 mali ya Kanisa la Kiinjiri Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbagala, jijini Dar es Saalam umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, alitoa kauli hiyo katika Mhakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Aloyce Katemana, wakati shauri hilo lilipotajwa.

Wakili Kweka aliiomba mahakama kutaja tarehe kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali, ambapo ilipangwa Desemba 24, mwaka huu. Aidha aliomba mahakama hiyo kuhamia eneo la tukio ili washtakiwa hao wasomewe maelezo yao wakiwa hapo na alikubaliwa.

Katika hatua nyingine MKurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewafutia mashtaka washtakiwa sita wa kesi hiyo kwa kutumia  mamlaka aliyopewa kisheria na kuongeza washtakiwa wengine watano.

Washtakiwa waliofutiwa mashtaka ni Mahenga Yusufu, Ramadhani Salum, Kasim Juma, Hatibu Abdalah, Hamad Mohamed na Mshamu Mwalimu. Walioongezwa ni Majembe Julius, Hamed Salehe, Shaban Mzee, Kambi Haji na Issa Abdalah.

Baada ya kufanya mabadiliko hayo,washtakiwa hao walisomewa upya mashtaka yanayowakabili ambayo ni kula njama,kuvunja jengo kwa nia ya kutenda kosa,kuharibu mali za zenye thamani ya sh.milioni 500 za KKKT Usharika wa Mbagala, unyang'anyi wa kutumia silaha na kuchoma Kanisa la KKKT usharika wa Mbagala. Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo.

No comments:

Post a Comment