24 December 2012

Dkt. Shein: Zanzibar inathamini ushirikiano wa Korea


                                                 
Na Rehema Maigala

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea, Bw.Chung IL, na kumueleza kuwa hatua ya nchi hiyo kuunga mkono kilimo cha mpunga wa umwagiliaji ni busara na ya kupongezwa.


Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana ilisema kuwa Dkt. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano kati yake na nchi hiyo na uamuzi wa Korea wa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa cha umwagiliaji  ni uthibitisho wa wazi wa ushirikiano.

Ilisema katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Dkt. Shein alitoa pongezi kwa Korea kwa hatua yake hiyo na kueleza kuwa juhudi hizo ndio chachu kwa Zanzibar katika kuzidisha azma yake ya kutekeleza mapinduzi ya kilimo.

Ilisema taarifa kuwa Dkt. Shein pia, alimpongeza Balozi huyo kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo kilimo.

Dkt. Shein alimueleza balozi huyo kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kimetiliwa mkazo mkubwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na katika kufanikisha azma hiyo mikakati kabambe imewekwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuanisha mabonde 57 yenye hekta 8,521 ambazo zinaweza kutumika katika kilimo hicho.

Taarifa ilisema tayari zaidi ya hekta 700 zilizomo katika eneo hilo zimeshawekewa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Korea ambapo jumla ya hekta 2000 tayari zimeshafanyiwa tathimini ya kinifu.

Aidha Dkt. Shein aliunga mkono wazo la Korea la kutaka kuanzisha ushirikiano katika usafiri wa anga kwa kuleta ndege zitakazofanya safari moja kwa moja kati ya Korea na Zanzibar kupitia Mashirika ya nchi hiyo.

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia katika kuzidisha ushirikiano sambamba na kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini kwa kuweza kupata watalii wengi kutoka nchini humo.

Naye, Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania alimueleza Dkt. Shein kuwa mradi huo wa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji mchakato wake unakwenda vizuri na unatarajiwa kuanza wakati wowote.

Hata hivyo taarifa hiyo ilisema kuwa balozi huyo ambaye amekuja kujitambulisha kwa Rais, alimueleza Dkt. Shein kuwa Korea itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo kilimo, na kusisitiza kuwa nchi yake kupitia ubalozi wa nchi hiyo utachukua juhudi katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Pia taarifa ilisema kuwa katika mazungumzo hayo  Balozi Chung alimueleza Dkt. Shein kuwa nchi yake itaangalia uwezekano wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja hadi Zanzibar kupitia mashirika yake ya ndege kwani tayari hivi karibuni imeshaanzisha nchini Kenya.

Aidha taarifa ilisema kuwa , Balozi huyo alipongeza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo huku akipongeza amani na utulivu iliyopo nchini na kupongeza juhudi za Dkt. Shein katika kuhakikisha amani na utulivu huo.

No comments:

Post a Comment