24 December 2012

China mbioni kutaka kutawala Uchumi



Na Danny Matiko

WIKI iliyopita katika makala haya tuliona Taifa la China likiwa limeshika nafasi ya pili ya ubora wa uchumi duniani, baada ya kuipiku Japan ambayo awali ilikuwa ikishikilia nafasi hiyo tangu mwaka 1968.


Marekani ambayo ni kinara bado inaendelea kuwa ya kwanza, ingawa pia watalaamu wa masuala ya uchumi, ikiwemo Benki ya Dunia, wanakadiria kuwa kati ya mwaka 2025 na 2030 huenda China itakuwa tayari imeshika hatamu na kuisukuma Marekani mpaka nafasi ya pili.

Katika sehemu hii ya leo, pamoja na mambo mengine, tutona jinsi "Jamhuri ya China" ilivyobadilika kuwa "Jamhuri ya Watu wa China."

Fuatilia kwa makini kwa kuwa mabadiliko hayo ndiyo kitovu cha siri ya maendeleo ya nchi hiyo ambayo tunataka kuibaini.

Kuibuka kwa China kuwa tajiri na kuelekea kukamata uchumi wa dunia ni historia ndefu na funzo kwa nchi masikini, zikiwemo za Afrika ya Mashariki, ambazo maendeleo yao ya kiuchumi yamekwama kusonga mbele kwa haraka.

Pengine jambo muhimu kwako Msomaji kufahamu mapema ni kwamba matukio ya kivita tunayoyaona sasa yakiendelea kujitokeza nchini Somalia, DR-Congo na kwinginepo Barani Afrika, ndiyo yalisambaratisha maendeleo ya China karne zilizopita.

Kabla ya hapo nchi hiyo ilikuwa na nguvu za kijeshi, kisiasa na kiuchumi kuliko nchi nyingi duniani.

Ingawa kiwango cha teknolojia ya China wakati huo kilikuwa ni  duni ikilinganishwa na ya wakati huu, bado sayansi ya wakati huo iliifanya China kuwa mashuhuri kwa viwango vya wakati huo.

Mojawapo ya nukuu kutoka kumbukumbu za Shirika la Upelelezi la Marekani (CIA) zinaeleza kuwa, "kwa karne nyingi China iliibuka kuwa na kiwango cha juu cha maendeleo kuliko nchi zote duniani, huku ikitawala katika sayansi na sanaa mbalimbali za dunia."

CIA inaeleza kuwa "maendeleo yote hayo ya China yalisambaratika kuanzia karne ya 19 na kuendelea kufuatia kutoweka kwa amani nchini humo, ambapo nguvukazi ilielekezwa kwenye kujaribu kutatua vurugu za wenyewe kwa wenyewe, njaa kali iliyosababishwa na vita, maradhi na mauaji ya kimbari."

Kiini cha mazingira hayo, CIA inaendelea, ilikuwa ni "kugombea madaraka, ambapo pia baadhi ya makundi pinzani yalitaka nchi hiyo kuwa ya kifalme."

Hali hiyo ilisababisha kuibuka kundi la "Wababe wa Kivita" ambalo lilijitwalia maeneo makubwa ya Kaskazini mwa nchi, na hivyo kuigawa nchi hiyo katika pande za Kaskazini, Magharibi, Kusini, Mashariki, na Kati.

Utawala uliokuwa umejianzisha ulipo mji mkuu wa sasa, Beijing, ulijaribu kutaka kurejesha eneo la Kaskazini katika "Muungano" wa himaya zilizounda China, lakini bila mafanikio.

Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya China, Sun Yat-Sea, aliyetwala kwa miezi mitatu mwaka 1912, na pia Rais wa pili, Yuan Shikai, aliyetawala kwa miaka miwili, yaani 1915 na 1916, kila mmoja alijaribu kuiunganisha China bila mafanikio.

Kushindwa kwa serikali hizo kulipelekea Marekani kuombwa kuingilia kati mgogoro huo ili kuwasambaratisha hao wababe wa kivita, lakini nchi hiyo ilikataa pengine kwa kuona kulikuwa hakuna maslahi yoyote.

Historia hueleza kuwa "Marekani ilipuuza maombi hayo ya kutaka kuzima uasi wa wenyewe kwa wenyewe kwa kuwa ilikuwa na ajenda muhimu zaidi katika maeneo mengine ya dunia."

Usemi wa "akufaaye wakati wa dhiki ndiye rafiki wa kweli," ulijidhihirisha pale serikali ya China ilipoamua kuifuata Urusi ili isaidie kuwasambaratisha "wababe wa vita" na kurejesha utulivu.

Licha ya Urusi kukubali ombi hilo, lakini pia kabla ya kufanya lolote iliazisha mafunzo ya kijeshi, maarufu kama "mafunzo ya mgambo" kwa raia wa China, na pia ikaanzisha Chuo cha Kijeshi, ambapo ilidai kuwa hiyo ilikuwa ni mikakati ya awali katika kuwaandaa wapiganaji ili kwenda kuwakabili wababe wa kivita.

Mbinu iliyotumika ni ya kudai kuwa mafunzo hayo hayakuwa na itikadi wala kupendelea upande wowote, kwani wafuasi wa vyama vyote, yaani wa chama tawala cha "Nationalist" cha serikali, ambacho pia kilikuwa na nguvu za kisiasa na wafuasi wengi, na kadhalika wale wa chama "dhaifu" cha Kikomunisti, waliruhusiwa kwa pamoja kupata mafunzo hayo maalumu ya kizalendo tayari kwenda kuwakabili wababe wa kivita.

Historia inatanabaisha kuwa kukamilika kwa mafunzo hayo kuliwezesha wapiganaji kuwa mchanganyiko, chini ya udhibiti na uongozi wa Warusi, ambapo safari ya kuelekea Kaskazini ilianza.

Safari hiyo inajulikana kama 'Northern Expedition', yaani "Safari ya haraka kwenda Kaskazini."

 Safari hiyo ngumu ilianza Mei 1926 baada ya wapiganaji kuhitimu mafunzo, ambapo zaidi ya wanamgambo laki moja waliunda umoja uliojulikana kama Jeshi la Kimapinduzi la China (NRA).

NRA ilijumuisha wafuasi wa Chama cha 'Nationalist' ambacho kiliunda serikali ya China, na wafuasi wa Chama cha Kikomunisti cha China.

Kwa upande wa kule Kaskazini, Wababe wa Vita katika himaya tatu walipata taarifa za kuijiwa na jeshi kubwa na kuamua kuunda umoja wao ambao ulijumuisha wapiganaji laki 2 na nusu ili kuwakabili wavamizi kutoka upande wa serikali.

Jeshi la NRA pamoja na zana zao, chini ya uongozi wa majenerali wa Urusi, lilitumia miezi 6 kuweza kufika maeneo ya wababe wa kivita ambapo pande mbili hizo zilikabiliana katika mapambano yanayofahamika kama "Vita Kuu ya Wenyewe kwa Wenyewe China.

Kwa kuwa wapiganaji hao NRA walikuwa wameandaliwa vyema zaidi kijeshi na kizalendo dhidi ya upande wa waasi, waliweza kuwashinda wababe wa kivita, angalao kwa muda.

Ile hatua ya Urusi ya kuunganisha pande mbili zenye itikadi tofauti, yaani Chama cha 'Nationalist' na cha 'Kikomunisti' na kuunda NRA, ilibadilika kuwa hasi kwenye uwanja wa mapambano dhidi ya wababe wa vita.

Ni kwamba kufuatia ushindi mdogo uliopatikana dhidi ya wababe wa kivita ulitosha kuwahamasisha wafuasi wa chama tawala cha "Nationalist" kugeuka ghafla kwenye uwanja wa vita na kuanza  kuwashambulia wafuasi wa chama cha "Kikomunisti" hukohuko vitani Kaskazini.

Mvurugano ulizuka huo uliwalenga wanamgambo wafuasi wa Kikomunisti ili "kuwafuta" kutoka jeshini katika uwanja wa vita.

Madhara yake yalisababisha wapiganaji wa upande wa wababe wa kivita kupata nguvu mpya na kuibuka, ambapo hali hiyo ilipelekea pande zote tatu kupigana dhidi ya kila mmoja na kuzuka utata mkubwa.

Kufuatia kubadlika ghafla kwa sura nzima ya hali ya mambo vitani, ambapo wapiganaji wa Kikomunisti walisakwa na kuuawa, Mao Zedong, mtoto wa mkulima, ambaye kabla ya kwenda uwanja wa mapambano alikuwa akifanyakazi katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Peking, aliamua kujitenga.

Mao akiwa na wafuasi wenzake wa Kikomunist wanaodhaniwa kuwa elfu 90 waliamua kutorokea upande wa Kaskazini-Magharibi ulipo mpaka wa China na Urusi.

Ingawa utorokaji huo uliwanusuru akina Mao, lakini pia jumla ya wenzake wapatao takribani elfu 70 walipoteza maisha wakiwa njiani kukimbia kuelekea mpakani mwa nchi yao na Urusi.

Matembezi hayo ya masafa marefu ya kujinusuru hujulikana kama "The Long March," ambapo inakadiriwa kuwa Mao na wenzake walitembea kuwakimbia wapiganaji wa Chama cha 'Nationalist' kwa umbali wa kilometa 12,500 kwa siku 370 bila kupumzika.

Katika matembezi hayo wengi wa walipoteza maisha kutokana na ajali mbalimbali, ikiwemo kuzama majini, kuangukia mabondeni wakati wakipanda milima, kuumwa na nyoka, njaa, kiu, na uchovu,

Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment