24 December 2012
Malumbano ya wanasiasa yanachanganya wapigakura
Na Esther Macha
NI muda mrefu sasa kumekuwepo na malumbano ya kisiasa baina ya mahasimu wawili ambao ni makada wawili wa chama cha mapinduzi (CCM), Mary Nagu na waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye ambao wamekuwa wakituhumiana jambo ambalo ni aibu kwa viongozi kama hawa kutuhumiana kwa rushwa.
Uchaguzi kama umeisha kuna sababu gani za kuendelea na mvutano usiokuwa na maana wakati kuna kero nyingi ambazo wananchi wanatakiwa wasaidiwe kupitia viongozi wao, huo muda wanaotumia kulumbana kwanini wasiende vijijini kuangalia kero za wananchi ,ni jambo ambalo linapaswa kufika mwisho sasa watanzania wamechoka na makada hawa.
Kwa jinsi ninavyoona uongozi wa sasa katika nchi masikini kama zetu ni tabu sana kwa kiongozi kama Sumaye ambaye alikuwa mtu mkubwa katika nchi kwanini asipumzike na kubuni kitu kingine cha msingi akafanya kuliko malumbano ya sasa anayofanya na kada mwenzake.
Kuna kazi nyingi za kufanya kwanini ajiweke zaidi kwenye siasa hasa kwenye ujumbe wa halmashauri kuu NEC kwani kuna nini huko ambako kunasababisha mpaka watu wawekeane chuki kubwa kiasi hicho.
Mimi binafsi najiuliza kuna kitu gani ndani ya chama cha mapinduzi mpaka kuwe na ugomvi mkubwa kiasi hiki ambao hata dalili ya kusema utakuja kuisha haupo , Sumaye na Nagu wote ni watu wazima kwanini wanaendeleza ugomvi usioisha.
Hii hali kwa kweli inachosha sasa ifike muda ifungwe na kujadili mambo mengine ya msingi maana sasa kila kukicha ni habari ya Sumaye na Nagu kiasi kwamba sasa wananchi wamechoka kusikiliza malumbano hayo ya kimaslahi ambayo yanadhoofisha maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Ninachoshauri kwa Bw.Sumaye apumzike siasa kwani miaka mingi aliyotumikia Taifa inatosha kwani yapo mazuri aliyofanya na mabaya aliyofanya ila agange yajayo.
Kiongozi wangu Sumaye kazi za kufanya za kijamii zipo nyingi hususani kufungua vituo vya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira kusaidia hilo pekee litakuwa msaada kwa Taifa kwani Taifa lina idadi kubwa ya watoto yatima ambao wanahitaji kusaidiwa.
Hili linalofanyika sasa ni aibu kwa taifa na wananchi ambao alikuwa akiwaongoza kuona kuwa kiongozi huyu yupo kimaslahi zaidi,hakuna sababu ya kuendelea na msuguano huu usiokuwa na mwisho wakati majukumu ya kufanya yapo mengi.
Ndo hapo sasa watanzania wanatakiwa kutambua kuwa asilimia kubwa ya viongozi wapo kimaslahi zaidi kuliko kuangalia kero za wananchi ambazo zinawasumbua huko vijijini , hebu fikiria uchaguzi wa viongozi wa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM (NEC) toka uishe ni zaidi ya miezi mitatu lakini makada hawa bado wanaendelea na malumbano makali ambayo hayana hata dalili ya kuisha.
Naamini kuwa katika uongozi wa Chama cha mapinduzi Taifa kuna viongozi wa juu ni jukumu lao sasa kuwaita makada hawa na kukaa nao kwa pamoja kulimaliza jambo hili ambalo halileti picha nzuri kwa Taifa letu , kwanza ni aibu kubwa sana hasa kwa waziri Mkuu mstaafu Bw. Sumaye hili ni baya linaleta aibu mbaya.
Tumeona mfano mkubwa kwa Mzee Mkapa rais mstaafu anafanya hayo kwa nini yeye asikae chini na washauri wake na kuacha na siasa kwani malumbano yamefanye apoteze mvuto kwa sasa ataishia kuaibika na kutafuta uchawi tu.
Lakini pia Kiongozi anapopatikana kwa rushwa, huongoza kwa rushwa kwani hawezi kuwa mshauri mzuri kwenye vita dhidi ya rushwa. Ambayo ndo imekuwa mwiba katika taasisi mbali mbali za kiserikali .
Uongozi ukimalizika au kushindikana kama wa Wazee wetu Sumaye na Mangula, ndio wanafunguka macho kuona machungu ya rushwa.
Hata Bi.Mary Nagu, siku ikifika rushwa ikimuangusha, atalia kwa uchungu na kujifanya mpambanaji jasiri dhidi ya rushwa wakati alishakosea toka awali hivyo kila kiongozi anapaswa kuingia madarakani kwa kutotumia rushwa kwani matokeo yake ndo kama hayo.
Hivi karibuni Sumaye ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu na Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), wameingia katika mgongano na mgogoro huu ulishika kasi wakati wa uchaguzi wa kumpata mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa, kupitia Wilaya ya Hanang’ ambapo Sumaye alibwagwa.
Wawili hao hivi sasa wameingia kwenye mvutano mkali kwa kutamkiana hadharani kuhusu rushwa jambo si zuri mbele za jamii na Taifa.
Katika uchaguzi huo uliofanyika, Nagu alimshinda Sumaye kwa kura, na baadaye, waziri huyo Mstaafu aliibuka na kueleza kuwa kushindwa kwake kulitokana na rushwa iliyokithiri kwenye uchaguzi huo, ikiwa inasukumwa na makada kadhaa wa CCM.
Lakini hivi juzi tu Sumaye alirudia kuituhumu CCM kwa ufisadi na akaenda mbali zaidi kwa kuwataka wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), kupiga vita kwa nguvu zote matumizi a rushwa aliyeeleza kuwa hivi sasa, yamekithiri kwenye chaguzi za chama hicho.
Akizungumza kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Hanang’ uliofanyika juzi mjini Katesh, Sumaye alisema matumizi ya rushwa kwenye chaguzi za nafasi mbalimbali ndani ya CCM, yanatakiwa kupigwa vita na wanachama wa UVCCM, kwani vijana ndiyo jeshi la CCM linalotakiwa kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano.
Lakini pia katika hili Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula kwasababu ameingia madarakani anapswa kuingilia kati suala hili ili liweze kuisha kwani kwa staili hii inatia aibu kwa viongozi wakubwa kama hawa kugombana ndani ya miezi mitatu kisa maslahi ni aibu kubwa , nina imani kuwa Makamu Mwenyekiti amelikuta hili atalimaliza haraka kabla halijaota mizizi.
Nina imani kuwa suala hili sasa litafika mwisho na Bw. Sumaye nae akae na kutakari kwa kina juu ya malumbano haya kwani kama kiongozi mkuu mstaafu inampotezea sifa nzuri kama kiongozi mstaafu .
Nionavyo katika hili ni kwamba Bw.Sumaye anapaswa kubaki kama kiongozi mshauri wa chama wa masuala mbali mbali yanayotokea ndani ya chama lakini si kinachojitokeza sasa ni aibu kubwa kukaa na kugombea nafasi za uongozi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
KILA MTU ANA UHURU WA KUTOA MAWAZO YAKE NA AKIYATOA ANAPUNGUZA STRESS ,FRUSTRATION NA KADHALIKA WACHOCHEZI NI VYOMBO VYA HABARI INASIKITISHA HABARI ZA UMBEA ,UDAKU,UZUSHI WA TANZANIA NDIZO ZINAZOUZA MAGAZETI
ReplyDelete