03 December 2012
Asisitiza matumizi ya chanjo mpya
Na Yusuph Mussa, Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, amewataka viongozi wa dini nchini kuwaelimisha
waumini wao ili wazingatie matumizi ya chanjo mpya
inayozuia watoto kuharisha na ile ya nimonia.
Alisema upo umuhimu wa jamii kuachana na dhana potofu iliyojengeka kuwa, chanjo zinazoletwa nchini zinazuia watu kuongezeka.
Bw. Gambo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa utambulisho wa chanjo hizo, ambapo Kamati ya Afya ya Msingi
ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe ilishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kuelezea faida ya kuwapa chanjo watoto wadogo.
“Tunaomba viongozi wa dini wawajibike kuwaelimisha waumini wao kuwa chanjo hii ni muhimu kwa ajili ya watoto wetu ili waondokane na fikra potofu kuwa chanjo zinazoletwa nchini zinasababisha ugumba,” alisema Bw. Gambo.
Aliwahadharisha watumishi wa afya na kuwataka wasiamini takwimu zinazotolewa bila kuzifanyia kazi kwa kina, ikibidi
waende vijijini na mitaani mara kwa mara ili kupata ukweli
wa takwimu hizo na kutoa huduma sahihi kwa watoto.
Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri ya mji huo, Dkt. Joyceline Sambo, alisema chanjo ya kuzuia kuhara inayoitwa 'Rotavirus', itawasaidia watoto wadogo na wenye umri kati ya wiki sita hadi 32.
“Chanjo ya nimonia ambayo inafahamika kama Pneumococcal Conjugate Vaccine (PCV), itawasaidia watoto kubanwa kifua
mara kwa mara na chanjo zote ni za kunyweshwa matone,”
alisema Dkt. Sambo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment