13 December 2012
Aliyetumwa kuua ashambuliwa na kuuawa
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Simiyu, likiwemo la mkazi wa Kijiji cha Kidalimanda, wilayani Bariadi, Marco Ntegwa (25), kushambuliwa na wananchi akituhumiwa kukodiwa ili kufanya mauaji kijijini hapo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Venance Kimario, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 7 mwaka huu, saa nane usiku kijijini hapo wakazi wa kijiji hicho kupata taarifa za Ntegwa kutaka
kufanya mauaji ya mkazi wa kijiji hicho.
“Siku ya tukio, wakazi wa kijiji hiki walipata taarifa kuwa Ntegwa pamoja na wenzake wawili walikodiwa na watu wasiojulikana kwenda kumuua Bw. Masanja Gumanda (52), ambaye ni mkazi wa kijiji hiki lakini walikosea nyumba na kuingia kwa Bw. James John.
“Bw. John na familia yake walipiga yowe la kuomba msaada ndipo wakazi wa kijiji hiki walifanikiwa kumkamata Ntegwa na wenzake wawili walikimbia, baada ya kuhojiwa alitoa siri hii, wananchi walimshambulia hadi kumuua na kumchoma moto,” alisema.
Alisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambapo polisi wanaendelea na uchunguzi pamoja na kuwasaka watuhumiwa wawili waliowahi kutoroka kabla ya kukamatwa.
Katika tukio jingine, mwanafunzi wa darasa la pili anayesoma Shule ya Msingi Nguno, Wilaya ya Itilima, mkoani humo, Pili Magani mwenye umri wa miaka minane, ameshambuliwa na fisi na kufariki dunia wakati akienda shuleni pamoja na mwanafunzi mwenzake.
Kamanda Kimario alisema, tukio hilo lilitokea juzi saa moja asubuhi ambapo marehemu aling'atwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Aliongeza kuwa, wakati fisi huyo akimng'ata marehemu, mwanafunzi mwenzake alikimbia na kupiga kelele za kuomba
msaada ndipo wananchi walitokea na kufika eneo la tukio lakini walikuta fisi huyo tayari amekula sehemu za mwili wa marehemu.
Alisema hivi sasa wananchi kwa kushirikiana na askari wanyamapori wanaendelea kumsaka fisi huyo ili waweze
kumuua asiendelee kuleta madhara kwa watu wengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment