13 December 2012

Ajali yauwa watano


Na Heckton Chuwa, Moshi

WATU watano wamefariki duniani katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, baada ya magari mawili kugongana katika eneo la daraja la Kikavu.


Kamanda wa Polisi mkoani humo, Robert Boaz, alisema ajali hiyo ilitokea saa 2:30 usiku ikihusisha gari lenye namba za usajili T 771 AQD, aina ya Toyota Hiace lori lenye namba T 212 AHH, aina ya Scania ambalo lilikuwa na tela lake namba T 653 AAJ.

“Gari aina ya Toyota Hiace ni mali ya Shule ya Scolastica iliyoko Himo, Wilaya ya Moshi Vijijini,, ambayo ilikuwa ikitokea Arusha kwenda Moshi, lori lilikuwa linatokea Moshi kwenda Arusha.

“Katika ajali hii, watu watano walijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, iliyoko mjini Moshi,” alisema.

Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Ernest Ambani, Bernard Omukunyu, Julius Kimario na Nelly Sasaka, wote walimu wa shule hiyo na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Opoloti.

Kamanda Boaz alisema, Jeshi la Polisi mkoani humo tayari limeanza uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo pamoja na kutoa wito kwa madereva kuwa makini katika kipindi hiki.

No comments:

Post a Comment