28 December 2012

Aangukiwa na ngozo ya umeme, afa



Na Omary Mngindo, Kibaha

MKAZI wa Kata ya Mlandizi, Wilaya ya Kibaha vijijini, mkoani Pwani, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na nguzo ya umeme.


Katika tukio hilo ambalo lilitokea Desemba 26 mwaka huu, saa tisa alasiri, marehemu aliyefahamika kwa jina la Said Mwakwaluzo (17),
ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Dosa Azizi, alikuwa na wenzake wawili.

Akizungumza na gazeti hili, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mlandizi, Dkt. Muhsin Issa, alisema marehemu alifikishwa katika hospitali hiyo akiwa kwenye hali mbaya na kufariki muda mfupi.

“Desemba 26 mwaka huu, saa 9 alasiri tulipokea vijana wawili ambao hali zao zilikuwa mbaya baada ya kuangukiwa na nguzo
ya umeme, pia walishambuliwa na nyuki ambao walikuwa
ndani ya nguzo hiyo,” alisema Dkt. Issa.

Majeruhi wa tukio hilo, Jackson John (17), alisema siku ya tukio, walikuwa watatu wakiwa wamekaa jirani na nguzo hiyo na kujikuta wameanguka, kushambuliwa na nyuki.

“Tulikuwa mimi, Mwakwaluzo na Abdul Ndenda, mwenzetu alituaga na kuondoka, baada ya kuanguka nguzo ilinibana miguu, mwanzangu ikambana kifuani tukawa tunapiga kelele huku nyuki wakitung’ata sehemu mbalimbali za mwili,” alisema John.

Aliongeza kuwa, wakati huo walishindwa kujinasua kutokana na kukosa nguvu kwani walikuwa wameshapoteza fahamu lakini watu walifika kuwaokoa baada ya kusikia kelele za kuomba msaada.

Kwa upande wake, Baba wa marehemu Bw. Shomali Mwakwaluzo, alisema mwanawe alikuwa anasoma kidato cha tatu shuleni hapo.

Jeshi la Polisi mkoani humo limekiri kupokea taarifa za kifo hicho na wanaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo.


No comments:

Post a Comment