28 December 2012

Tanzania yaunga mkono tamko la uchunguzi ujangili wa tembo


Na Mwandishi Wetu

TANZANIA inaungana na Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa linalojihusisha na kulinda wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani (CITES), Bw. John Scanlon, kuunga mkono tamko la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu tuhuma zinazodai kundi la waasi nchini Uganda la Lords Resistance Army (LRA), linajihusisha na ujangili wa tembo.

Kundi hilo pia linadaiwa kuhusika na usafirishaji wa meno yake
ili kupata silaha na fedha za kugharimia shughuli zake za uasi.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema tamko hilo hilo limeongeza nguvu juu ya hisia iliyopo kuwa kuna uhusiano kati ya ujangili na hali ya usalama katika eneo la Maziwa Makuu na Afrika ya Kati.

Alisema wiki iliyopita, baraza hilo lilitoa tamko ambalo liliutaka Umoja wa Mataifa (UN( na Umoja wa Afrika (AU), kulichunguza kundi hilo jinsi wanavyopata fedha za kununulia silaha na kuhusika kwao katika ujangili wa tembo na usafirishaji meno yake.

“Baraza lilijulishwa kuwa, LRA wanafanya vitendo vya kusafirisha meno ya tembo na kupanua maeneo wanayofanyia ujangili, hivi sasa ujangili wa tembo, faru na biashara haramu ya meno yao, imeongezeka katika mataifa mengi ya Afrika.

“Kama ilivyosisitizwa na CITES, mauaji ya tembo wengi kwa
ajili ya meno yao yanafanywa na makundi ya waasi ambayo yaliyojipanga vyema kwa kutumia silaha nzito,” alisema.

Balozi Kagasheki aliongeza kuwa, CITES limebaini kuwa meno yanayotokana na ujangili unaofanyika katika eneo la Maziwa Makuu na Afrika ya Kati, yanasadikiwa kufanywa na waasi ili kujipatia
fedha, silaha na risasi kwa ajili ya kuendeleza machafuko kati
ya nchi mbalimbali jirani.

Alisema Tanzania iko tayari kufanya kazi na Umoja wa Mataifa katika uchunguzi unaohusu ushiriki wa wapiganaji kufanya
ujangili wa wanyamapori.

“Sisi tunaamini kuwa, uchunguzi huu utabaini wahusika wakuu wa kimataifa katika biashara ya meno ya tembo na mwenendo wake ulivyo sasa, uchunguzi huu utafanyika sambamba na juhudi zinazoendelea nchini za kupigana na ujangili,” alisema.

Wakati huo huo, Tanzania inajadiliana na wadau mbalimbali ili Kongamano la Kimataifa kuhusu Ujangili liweze kufanyika nchini
mwaka 2013. 

Kongamano hilo litahudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka barani Afrika wanaoathiriwa na wimbi lisilokubalika la ujangili unaohusiana na meno ya tembo na faru.

Lengo la kongamano hilo ni kujadili kwa kina, kubadilishana
uzoefu na kutafuta ufumbuzi dhidi ya ujangili.

No comments:

Post a Comment