28 November 2012

Wizara yawapeleka wakulima 14 katika maonesho ya kilimo SudanNa Mariam Mziwanda

WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika, imewagharamia wakulima kutoka mikoa tisa nchini kwenda nchini Sudan ili
kushiriki maonesho ya kilimo.


Akizungumza Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya kuwaaga wakulima hao, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, alisema wakulima hao wanapaswa kujivunia
fursa hiyo ili kujiwekea mazingira ya kuuza bidhaa zao nje.

Alisema amesikitishwa na taarifa zinazodai wafanyabiashara kutoka nchi jirani, hupeleka mazao yanayolimwa Tanzania nchini Sudan bila wakulima wenyewe kunufaika na mazao hayo.

“Niliwahi kukutana na Waziri wa Kilimo nchini Sudan akanieleza kuwa, kuna mazao mengi hasa ya chakula ambayo hayauzwi na Watanzania bali yanauzwa na wanunuzi kutoka nchi jirani.

“Ili wanunuzi hao waweze kuingia kwa urahisi nchini Sudan, wanatumia namba za magari ya Tanzania, hali hii inawafanya
wauze vyakula kwa wingi na kupata faida kubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, kutokana na raia wa Sudan kuhitaji zaidi mazao
ya Tanzania yenye ubora mkubwa, wanunuzi wengi kutoka nchi
jirani hununua mazao hayo kwa bei isiyowanufaisha wakulima.

Mhandisi Chiza alisema,baada ya kubaini hali hiyo ameona ipo haja ya kutumia mwaliko wa maonyesho hayo nchini Sudan kupeleka wakulima wadogo na wafanyabiashara ili kwenda kujifunza na kutafiti namna ya kunufaika na fursa hiyo.

Alisema kutokana na ukubwa wa maeneo ya kilimo nchini na elimu ambayo wataipata wakulima hao, itawawezesha kuongeza ufanisi na tija ya uzalishaji vyakula.

Aliongeza kuwa, upo umuhimu wa kujifunza vikwazo vya kibiashara na aina ya mazao yanayohitajika kwa wingi ili
kuyapatia masoko na kuyasindika katika ubora unaotakiwa.

Akizungumza na gazeti hili, mkulima kutoka mkoani Katavi, Bw. Wiliam Mbogo, aliishukuru Serikali kwa kuwapa kipaumbele ili waende kujifunza kilimo chenye tija.

“Katika safari hii, tutatumia ushiriki wetu kuongeza msukumo wa kushiriki katika biashara za pamoja,” alisema Bw. Mbogo.

Safari hiyo ya siku tano, itawahusisha wakulima 14 kutoka mikoa ya  Kigoma, Iringa, Rukwa, Katavi, Kagare, Dodoma, Morogoro, Arusha na Kilimanjaro, ambao wataongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali.

No comments:

Post a Comment