28 November 2012
Mbunge CCM alalamika kupigwa vita
Na Yusuph Mussa, Korogwe
MBUNGE wa Korogwe Vijijini, mkoani Tanga, Bw. Stephen Ngonyani (CCM), amesema baadhi ya wanachama wanzake
wanampiga vita kwa kukataa kutangaza miradi anayoipeleka
katika kata zao.
Alisema sababu ya wana CCM wenzake kufanya hivyo ni hofu waliyonayo kuwa watakuwa wanampigia debe aendelee kuwa mbunge katika kipindi kingine cha miaka mitano.
Bw. Ngonyani aliyasema hayo juzi katika sherehe za Benki ya Wananchi Vijijini (VICOBA), ambapo Kikundi cha Muungano kilichopo Kitongoji cha Mlembule katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mombo, walikuwa wakivunja 'kibubu' na kugawana fedha zao.
Alisema katika maeneo aliyopeleka miradi ya maendeleo na
kushindwa kutangazwa kuna wagombea ubunge walioshindwa
katika kura za maoni ndani ya chama hicho mwaka 2010.
Aliongeza kuwa, kikwazo cha miradi hiyo kutotangazwa katika
kata 20 jimboni humo kimechangiwa na madiwani ambapo hali
hiyo ni kutaka wana CCM hao 'kujikomba' kwa mmoja kati ya wagombea ubunge mtarajiwa katika Uchaguzi Mkuu 2015.
“Baadhi ya viongozi kwenye vijiji na kata wanashindwa kutangaza kazi nilizofanya na miradi ya maendeleo ninayoipeleka kwenye maeneo yao eti wataonekana wananipigia debe niendelee kuwa Mbunge wa jimbo hili.
“Kimsingi wanataka kujipendekeza kwa baadhi ya wagombea ubunge, nasema mimi ndiyo Mbunge wa Korogwe Vijijini kwa
sasa hivyo wana CCM na wananchi wanatakiwa kulijua hilo
pamoja na kunipa ushirikiano,” alisema.
Katika sherehe hizo Bw. Ngonyani aliahidi kutoa sh. 500,000 kwa kikundi hicho kama sehemu ya mtaji wao, pamoja na mabati ya ujenzi wa ofisi yao na pampu kwa ajili kilimo cha umwagiliaji.
Pia Bw. Ngonyani aliahidi kutoa sh. 500,000 kwa Kikundi cha Umoja kilichopo Kitongoji cha Kwamgogo kwenye Mamlaka
ya Mji Mdogo wa Mombo, matofali ya sh. 300,000, ambapo
ahadi nyingine ni kutoa sh. 250,000 kwa Kikundi cha Muungano
ambazo zimetolewa na Mbunge wa Handeni Dkt. Abdallah Kigoda.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment