28 November 2012

Watu wenye ulemavu wapewe fursa ya ajira



Desemba 31 kila mwaka, Tanzania ni miongoni mwa nchi mbalimbali duniani zinazoadhimisha siku ya watu wenye
ulemavu.

Kauli mbiu mbalimbali huwa zinatumika katika maadhimisho
hayo kila mwaka ili kuleta mahasa ya kulinda, kutetea haki zao
na kuwajengea ustawi mzuri wa maisha yao.

Moja kati ya kauli mbiu hizo ni ile iliyosema “Malengo ya milenia yawe jumuishi, wezesha watu wenye ulemavu na jamii zao ulimwenguni'.

Serikali pamoja na wanaharakati, wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu nchini, zinapatikana kuanzia katika elimu na nyanja nyingine za kijamii.

Haki hizo ni pamoja na kuboresha majengo kwa kujenga sehemu maalumu ambazo zitatumiwa na watu wenye ulemavu kwa ajili ya kufuata huduma katika ofisi mbalimbali, kuwakilishwa katika vyombo vya kiserikali na haki nyingine za msingi.

Mei 8, 2008, Umoja wa Mataifa (UN) na wanachama wa umoja huo, walilidhia mkataba unaotambua haki za watu wenye ulemavu ambao ni zaidi ya milioni 650 duniani kote.

Sisi tunasema kuwa, watu wenye ulemavu bado wana safari ndefu ya kuhakikisha haki zao zinalindwa na kuheshimika kwa mujibu wa sheria wakiwa na uhuru kamili wa kujieleza na kushiriki kwenye maisha ya hadhara.

Kati ya mambo muhimu yaliyopo katika mkataba huo ni mkazo uliowekwa juu ya usalama wa mtu binafsi, haki ya maisha na dhamana ya Serikali kwa ajili ya kuwasaidia ili waweze
kupambana na umaskini.

Mambo yote haya ni muhimu ili kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia ikiwa ndio sababu ya nchi wanachama wa UN, kuridhia mkataba huo na kuweka saini ili uanze kutumika mara moja.

Haki za msingi ambazo watu wenye ulemavu walikuwa wakizikosa, hivi sasa wameanza kuzipata kama njia moja wapo ya kutekeleza mwongozo wa mkataba huo ingawa bado hatujafikia hatua
kubwa ya mafanikio kama inavyokusudiwa.

Tatizo kubwa linalojitokeza sasa ni fursa ya ajira kwa watu wenye ulemavu. Wapo waajiri wachache wanaokubali kuajiri watu wenye ulemavu lakini wengi wao, wamekuwa na dhana tofauti.

Wapo waajiri wanaoamini watu wenye ulemavu hawana uwezo wa kufanya kazi, kuchangia maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.

Hali hii inachangia idadi kubwa ya watu wenye ulemavu, kuishi mitaani wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha ingawa baadhi
yao wamejitahidi kusoma kwa uwezo waliofikia.

Kuna kauli inayosema kuwa, watu wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kujiletea maendeleo hivyo ni wajibu wa waajiri kuona umuhimu wa kuwapa nafasi za ajira ili kuleta usawa katika jamii.

Ni wazi kuwa, katika suala la ajira walemavu wameachwa nyuma sana hali inayowafanya wakate tamaa na kuona bado wanatengwa katika jamii.

Ni vyema kwa kila mwanajamii, awe mstari wa mbele kutetea na kusimamia haki za msingi za watu wenye ulemavu kwa waajiri ili waweze kupatiwa ajira ambazo ndio zitawakomboa kimaisha na kuharakisha maendeleo yao.

Ukweli ni kwamba, kundi kubwa la watu wenye ulemavu wana sifa za kuajiriwa na kufanya kazi ofisini sawa na watu wasiokuwa na ulemavu ila wameshindwa kupata kazi kutokana na hali zao.

No comments:

Post a Comment