28 November 2012

Abood lapata ajali, lajeruhi wanafunzi 7



Rehema Maigala na Rose Itono

WANAFUNZI saba wa Shule ya Awali ya Mount Moria, iliyopo Kibamba, Dar es Salaam, wamejeruhiwa baada ya basi la shule walilokuwa wamepanda kugongwa na basi la Kampuni ya Abood, ambalo lilikuawa likitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro.


Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa, dereva wa basi la Abood aliyejulikana kwa jina la Bw. Sadick Mtwange, anashikiliwa polisi.

Kamanda Kenyela alisema basi lililosababisha ajali lina namba za usajili T 527 AZE aina Scania, ambalo baada ya kufika maeneo ya Kibamba Hospitali, liliyapita magari mengine na kwenda kuligonga basi la shule lililobeba wanfunzi ambalo lilikuwa limesima.

Alisema basi la wanafunzi lenye namba za usajili T 232 BQH,
aina ya Toyota Hiace, ambalo lilikuwa kituoni likipakia wanafunzi,
kugongwa ubavuni na kusababisha liingie mtaroni.

Aliongeza kuwa, wanafunzi hao walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha, mkoani Pwani, kupatiwa matibabu.

Aliwataja wanafunzi waliojeruhiwa kuwa ni Mtoni Fotuna (5), Diana Tarimo (6), Beatrice Msambusi (5) Layani Agustino (6), Gladnes Lusekeno (10), Husein Mjeku (6) na Brayan Shumo (5).

Kamanda Kenyela alisema hali za wanafunzi hao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu ambapo dereva wa basi hilo alishindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

No comments:

Post a Comment