27 November 2012

Wassira awataka viongozi CCM kutatua matatizo ya wananchi


Na Raphael Okello, Bunda

MBUNGE wa Bunda, mkoani Mara, Bw. Stephen Wassira, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimefanya kazi
kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo lakini bado
kinakabiliwa na matatizo mbalimbali.


Alisema baadhi ya matatizo hayo ni viongozi kutumia fedha ili kununua uongozi ndani ya chama na kushindwa kuwa karibu na
wananchi, kusikiliza kero zao mambo ambayo hivi sasa chama
hicho kimeanza kuyafanyia kazi.

Bw. Wassira aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wana CCM pamoja na viongozi wa chama hicho wilayani humo baada
ya kupokelewa na kumpongeza kwa kupata ujumbe wa NEC Taifa, katika uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni..

“Lazima viongozi wa CCM katika ngazi zote wawe karibu na wannchi pamoja na kusikiliza kero zao, kama kuna makundi
ndani ya chama kutokana na chuki za walioshindwa ni vyema tujiangalie upya na kutafuta ufumbuzi wa tatizo.

“Makundi haya yanaendelezwa na wagombea walioshinda nafasi walizoomba ndani ya chama, umefika wakati wa kuyavunja na kuendeleza mshikamano,” alisema Bw. Wassira.

Aliwapongeza wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa CCM kwa kumpigia kura na kujigamba kuwa, ushindi huo umechangiwa na
uadilifu wake katika kuwatumikia Watanzania.

“Wapo wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wanalalamika na kudai vyombo vya dola haviwatendei haki pamoja na kusuasua kwa huduma za jamii, je, viongozi wa CCM katika maeneo husika mnachukua hatua gani.

“Tusizibe masikio kwa kujivunia mafanikio tuliyonayo kama chama bali tusikilize na kuchukua hatua pale tunapoletewa malalamiko la sivyo wananchi watapoteza imani chama chetu na kuwapa dola wapinzani,” alisema Bw. Wassira.

Hata hivyo, Bw. Wasira alitamba na kudai kuwa safi mpya ya CCM imeamua kuwaeleza Watanzania ukweli wa mafanikio yaliyofikiwa na nchi pamoja na mikakati iliyopo kushughulikia kero zilizopo.

“Jeshi lolote linafanya mazoezi makali kabla ya vita ili liweze kumshinda adui, wakati wa vita hivyo CCM imeamua kwenda
kwa wananchi kabla ya uchaguzi ili iweze kushinda,” alisema.

Aliongeza kuwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), bado hakina uwezo wa kuongoza nchi kwani
ina safu ndogo ya viongozi wanaotawaliwa na ukanda.

“Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, anadai sera ya elimu bure imetolewa na chama chao si kweli, hii ni sera ya CCM.

“Dkt. Slaa ni muongo sana, tena mwenye tabia ya kuzua mambo kwani sisi tunaamini kuwa sera ya elimu bure ni ya CCM si chama
kingine cha siasa kama wavayodai CHADEMA,” alisema na kudai kuwa, Slaa pamoja na Mbowe, wote walisoma bure kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere, sera ambayo inaendelea hadi sasa.

Bw. Wassira ameanza ziara jimboni kwake ili kusikiliza kero za wananchi na kuelezea mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya CCM.

1 comment:

  1. Mzee wa gombe anazeeka bure, atwambie ni shule gani sasa ya serikali wanafunzi wanasoma bure bila kulipia kidato cha kwanza hadi cha nne?

    ReplyDelete