21 November 2012

Wanafunzi wanapotoshwa masomo ya sayansi



Na Kassim Mahege

MASOMO ya Sayansi ni miongoni mwa taaluma ambayo imeleta maendeleo makubwa ulimwenguni na kutufikisha katika karne ya Sayansi na Teknolojia ambayo hatimaye tunajivunia Utandawazi.


Katika,mitaala inayotumika kufundishia wanafunzi wetu wa Tanzania,imetoa fursa ya kipao mbele katika masomo ya taaluma ya sayansi,Biashara,Masomo ya sanaa nk.

Mwanafunzi anapoanza kidato cha kwanza mpaka kidato cha pili,mwanafunzi huyo hufundishwa masomo yasiyopungua 12 yakiwemo Fizikia, Baiolojia, Kemia na mengineyo.

Mara baada ya kumaliza kidato cha pili na kafanya mtihani wa Taifa ambao huandaliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE),mwanafunzi huyo hupata nafasi ya kuchagua masomo anayopenda kuyasoma maarufu kama(Combination) ikiwa ni maandalizi ya kuchagua taaluma atakayo kuisomea.

Utaratibu huo ni mzuri japokuwa kunajitokeza  tatizo pale inapotokea mwanafunzi huyo kusoma masomo zaidi ya saba,hali inayopingana na suala zima la kuchagua masomo na kusababisha wanafunzi hao kushindwa kumudu masomo yao waliyochagua kutokana na masomo kuwa mengi.

Sipendi kuzungumzia tatizo hilo kwa sababu sio mada yetu isipokuwa leo tutajikita katika suala la kufundisha masomo hayo kwa  maelezo peke yake bila  vitendo.


Kwa mwanafunzi anayesoma masomo ya Sayansi changamoto ya kwanza kubwa ambayo wanafunzi wengi zaidi hukutana nazo ni kukosa Maabara zenye vifaa  vinavyohitajika kwa ajili ya kujifunza  kwa vitendo.

Shule nyingi za Tanzania hususani shule za  Serikali ambazo ndizo zinazotumiwa na Watanzania wengi,zinakabiliwa na tatizo hilo mpaka imefikia hatua baadhi ya wanafunzi wanalalamika kuwa waalimu wao wanakataza kugusa vyombo hivyo pindi wanapokuwa katika maabara hizo ,kwa kuhofia kuwa vyombo hivyo vitaharibika.


“Tunaingia maabara mara moja kwa wiki,na ukiingia kuna baadhi ya vifaa unakatazwa kuvishika kutokana na gharama kubwa pindi vitakapo haribika”anasema mwanafunzi ambaye jina lake na shule tunalo.

“Nimelazimika kuhama masomo ya sayansi kwa sababu  unafundishwa nadharia bila vitendo ,sasa mimi nitakuwa mwanasayansi wa aina gani?”anahoji mwanafunzi huyo.

“Katika shule yetu tanayo maabara lakini kuna baadhi ya vifaa hakuna,hivyo kusababisha wanafunzi wengi kukataa kusoma masomo ya sayansi na kukimbilia masomo ya sanaa,”anaongeza

Kimsingi kwa hali kama hiyo ikiwa wanafunzi hawapati nafasi ya kushiriki kikamilifu kujifunza kwa vitendo,ndipo niliposhawishika kusema kuwa  wanafunzi wa kitanzania wanafundishwa historia ya sayansi na sio sayansi.

Masomo ya sayansi yanakwenda pamoja na  kujifundisha kwa vitendo,ikiwa masomo ya vitendo yanakosekana tunategemea kuwa siku mmoja katika nchi yetu watatokea wasomi wa fani hiyo kugundua  chombo chochote kama ilivyo kwa wasomi wenzetu kutoka nchi mbalimbali duniani ili ulimwengu ukafaidika kutokana na ugunduzi huo?

Tunafahamu kuwa maendeleo yote tunayoyaona hivi sasa ni kutokana na juhudi za wasomi wa taaluma hiyo ambapo walioandaliwa vizuri ikiwa ni pamoja  na kufundishwa kwa vitendo ndipo walipoweza  kugundua vyombo mbali mbali kama vile usafiri wa ndege,kompyuta,nishati ya umeme,vifaa vya mawasiliano na mitandao mingine,ambapo sasa dunia  imekuwa kijiji kimoja.

Au ndiyo tunaamini kuwa watanzania hatuwezi kugundua vitu vya msingi isipokuwa wazungu peke yao?

Msomi mmoja wa elimu ya sayansi ya jamii aliwahi kusema kuwa maendeleo yote tunayoyaona hivi sasa ni asilimia 20 ya akili ya mwanadamu ndiyo iliyotumika kugundua mambo yote tunayoyaona.


Kupitia kauli hiyo bado kiasi cha asilimia 80 ya akili ya mwanadamu bado haijatumika,hivyo kuna kila sababu kuondokana na mawazo mgando ya kuamini kuwa wazungu pekee yao ndiyo wenye uwezo wa kugundua mambo, hali ya kuwa wazungu wana uelewa sawa na sisi wakati mwingine sisi tunaweza kuwa  tuna uwezo mkubwa kuliko wao.

Athari kubwa inayopatikana kutokana na wanafunzi kukosa kujifundisha kwa vitendo ni pamoja na kudumaza ubunifu na uwezo wa mwanafunzi,hatimaye tunakuja kupata wasomi ambao sio wabunifu na mwisho wa siku maendeleo yanakosekana kwa taifa kutokana na wasomi wetu kukosa ubunifu na uwezo wa kufanya kazi.

Wakati mwingine ni busara kujipeleleza ikiwa ni pamoja na kujifanyia tathmini ili kubaini ni kwanini maendeleo yetu yamekuwa yakisuasua licha ya kuwa nchi yetu imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ambapo baadhi ya mataifa yanatushangaa kutokana na umasikini uliokithiri.

Ikumbukwe tatizo hilo haliishii kwa wanafunzi tu,isipokuwa tatizo hilo litakuwa linaendelea mpaka mwanafunzi huyo atakapokuwa mtaalamu wa fani fulani na mwendelezo wake na pale mtaalamu huyo kukabidhiwa jukumu la kuwatumikia wananchi kwa kukabidhiwa sekta yoyote ile.


Kwa mfano miongoni mwa viongozi wengi waliopewa majukumu katika utumishi wa umma ndiyo wale ambao waliosoma kwa utaratibu huo tulioueleza,je nchi yetu inaweza kupata maendeleo eti kwa sababu tu tunazo rasilimali nyingi nchini kwetu?

Kuna usemi usemao kwamba  kwenye miti hakuna wajenzi,haitoshi tuu kuwa na rasilimali nyingi ndiyo nchi inaweza kupata maendeleo,jambo la msingi ni kujiuliza kwa namna gani tunaweza kuziendesha rasilimali zetu ikiwa ni pamoja na kuwa na maarifa ya kutosha ili kuweza kuvuna kupitia wasomi wetu.


Kimsingi bado wahusika hawajaamuwa kuwawezesha  wanafunzi wetu wanaosoma masomo ya sayansi kupata taaluma hiyo ipasavyo,siamini kuwa serikali haifahamu tatizo la maabara kwa shule nyingi zilizopo nchini kwetu kuwa ni changamoto kwa taifa ,hivyo nichukue fursa hii kuwakumbusha  wadau mbalimbali wa elimu kuliangalia tatizo hilo kwa jicho la tatu ili kuondoa au kupunguza changamoto hiyo.

Siku zote unapotaka kutatua tatizo kwanza lazima  ujue chanzo chake,tunapozungumzia suala la  umasikini kwa wananchi ni vyema pia watendaji wa suala husika kuwatambua uwezo wao kutokana na majukumu yao waliyopangiwa wanayatekeleza kwa namna gani,ambapo udhaifu huo husababishwa na ufundishaji usiojali mafunzo ya vitendo na kupelekea kupata wataalamu wasiokuwa wazuri.

Tumezoea kusikia kuwa Serikali ikitoa kipau mbele kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya hesabati,hususani kwa wanafunzi wa kike na kusababisha wanafunzi wengi kupenda somo hilo.

Kumbe inawezekana kuwa kama Serikali pia ikatoa kipau mbele katika masomo ya sayansi kwa kuhakikisha kuwa inawawekea wanafunzi hao  maabara za kisasa pia itasaidia masomo hayo kupendwa  na wanafunzi wengi ili tuweze kupata wataalamu wengi wazuri.

Kutokana na uchunguzi wangu nimegundua kuwa wanafunzi wengi hawapendi masomo ya sayansi hususani wa kike hali ambayo inasababaisha pia washindwe kuyamudu, jee serikali inafanya nini ili kuwashawishi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanafunzi wetu wa kitanzania  kuyapenda  na kuyamudu masomo hayo?

Ifike mahali tujitambue kuwa sisi tuna uwezo  sawa na mataifa ya Magharibi hivyo Serikali iziwezeshe shule za sekondari kuwa na maabara za kisasa
pamoja na vitendea kazi vya kutosha ,ili Taifa lipate wanasayansi bora na  sio bora wanasayansi.

No comments:

Post a Comment