21 November 2012

Waathirika wa Kimbunga Mbagala walalamika kutotekelezewa ahadi


Na David John

WAKAZI wa Mbagala kwa Mangaya, Dar es salaam, ambao waliathirika na kimbuka kilichotokea mwaka 2011, wameitupia
lawama Serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi walizotoa
baada ya kaya 70 kubomolewa nyumba zao na nyingine
kuezuliwa paa zake kutokana na kimbunga hicho.


Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Diwani wa Kata ya Mbagala, Bw. Agrey Kayombo, aliiomba Serikali ione umuhimu wa kuwasaidia hao kwa kutekeleza ahadi walizotoa za kuwapatia bati ili waweze kuezeka katika nyumba hizo.

Akizungumza kwa niaba ya waathirika hao, Bw. Mohamed
Karrim alisema wanapata shida kwani kaya zote ambazo nyumba zao zimebomolewa na kimbunga hicho hivi sasa zinalala nje baada ya mahema waliyopewa na Serikali kupasuka na mengine kuchakaa.

“Tunaiomba Serikali itusaidie maana hivi sasa wametusahau mbali ya kutupa ahadi nyingi ikiwemo ya kupewa mabati na waathirika wengine waliofiwa na waume zao kujengewa nyumba lakini hadi
leo hakuna kilichofanyika,” alisema Bw. Karrim.

Alisema wakati kimbunga hicho kinatokea viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam walikwenda kushuhudia akiwemo Bw. Meck Sadick (Mkuu wa Mkoa), Mbunge wa Kigamboni, Bw.  Faustine Ndungulile na kuhaidi kutoa msaada wa mabati kupitia Mfuko wa Maafa lakini hadi sasa hakuna utekelezaji.

“Tunajua Serikali yetu ina mambo mengi lakini inapaswa kuangalia wananchi wake wanaopatwa na matatizo ambayo si yakujitakia kama hili la kimbunga,” alisema.

Kwa upande wake, Bw. Kayombo aliwataka waathirika hao kuunda kamati maalumu ya kufuatilia ahadi hiyo badala ya kulalamikia pembeni kwani Serikali ina mambo mengi.

“Ndugu zangu si kwamba jambo hili limepuuzwa bali mambo yaliingiliana, wakati Serikali ya Mkoa ikijipanga kutekeleza ahadi likatokea jambo jingine la mafuriko hivyo Serikali nzima ikawa imepeleka nguvu zake huko,” alisema Bw. Kayombo.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Mkoa ilijitahidi kutafuta njia ya
kuweza kupata fedha au mabati lakini bahati mbaya kilichopatikana kilikuwa kidogo hivyo ni muhimu kuunda kamati ambayo itasaidia kupata ufumbuzi wa tatizo lililopo.

No comments:

Post a Comment