21 November 2012

Wanafunzi 3 wafunikwa na kifusi, wafariki dunia


Na Eliasa Ally, Iringa

WANAFUNZI watatu wa Shule ya Msingi ya Kidamali, iliyopo Kijiji cha Kidamali, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, wamekufa baada ya kufunikwa na kifusi cha mchanga uliokuwa jirani na shimo.


Shimo hilo lilichimbwa na wananchi jirani na Kanisa la Othodocs,
ili waweze kupata mchanga wa kujengea nyumba zao.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Daima Luvanda, aliwataja wanafunzi waliokufa kuwa ni Nelsodi Luvanda (16) aliyekuwa akisoma darasa la sita, Owen Sanga (8) na Cheki Mbwilo (9), ambao wote walikuwa wakisoma darasa la kwanza.

Alisema siku ya tukio, mvua kubwa ilinyesha ambapo ambapo katika shimo hilo kulikuwa na watoto wengi na baada ya kuona
kifusi kimewafunika, wengine waliweza kujiokoa na kwenda
kutoa taarifa kijijini.

Aliongeza kuwa, baada ya kupata taarifa hizo, wananchi walikusanyika na kwenda kufukua miili ya marehemu
ambayo ilipelekwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya
Iringa Tosamaganga.

“Tukio hili lilikuwa la ghafla na limetushtua sana, tumeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa hivyo nawaomba wananchi
wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu.

“Kila mzazi ahakikishe anawajibika kuwalinda watoto wake ili wasicheze katika maeneo ya hatari,” alisema Bw. Luvanda.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nzihi, Bw. Stephani
Mhapa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, alisema tukio hilo wanafunzi hao wamepoteza maisha
katika umri mdogo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamhanda, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambalo uchunguzi wake bado unaendelea.


No comments:

Post a Comment