26 November 2012

Wana mazingira mko wapi mbona nchi inateketea?



Na Michael Sarungi

TAKWIMU zilizopo zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo kila ifikapo Juni 5 ya kila mwaka, huadhimisha siku ya mazingira.

Maadhimisho haya huwa ni sehemu ya kumbukumbu ya mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa UN, kuhusu mazingira uliofanyika mwaka 1972 mjini Stockholm, Swiden.

Katika mkutano huo, wadau wa mazingira walipitisha azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushugulikia mazingira (UNEP) na kauli mbiu yake ilikuwa ni, Viumbe ni wengi, dunia ni moja na mstakabali ni mmoja.

Pamoja na kuwa hadi sasa ni kipindi kirefu tangu kutangazwa kwa ujumbe huo, lakini bado unabeba ujumbe mzito katika Tanzania ya leo na dunia nzima kwa ujumla kwani maendeleo endelevu kwa kiwango kikubwa yanategemea jinsi tulivyo jipanga kulinda mazingira yetu.

Ingawa changamoto zinazotukabili ni nyingi, lakini tawimu zilizopo zinaonesha kuwa asilimia 60 ya nchi yetu inakabiliwa na hali ya  ukame uliokithiri.

Katika nchi ya Tanzania takriban hekta 220,000 za misitu huteketezwa kila mwaka kwa mahitaji ya nishati hususan mkaa, kilimo kisicho endelevu na biashara ya magogo.

Mbali na sababu hizo pia  malisho katika mikoa mingi yamezidiwa na wingi wa mifugo, hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na uvamizi wa vyanzo vya maji.

Kwa kiwango kikubwa mazingira ya bahari yanaharibiwa kwa kiwango cha kutisha hasa kwa kutokana na uvuvi usio kuwa endelevu na uchafuzi wa mazingira.

Kwa mfano takwimu zilizopo zinaonesha kushuka kwa wingi wa samaki wanaovuliwa baharini toka tani 52,935 mwaka 2001 hadi tani 43,459 mwaka 2007.

Kushuka huko ndilo jambo linalozua maswali mengiMOJA, Je! kama hali hiyo ilikuwa ni hivyo  miaka hiyo kwa sasa tuna hali gani?

Pili tukiacha hali kama hii ikaendelea itakuwa je! katika kipindi cha miaka 40 ijayo?.Tatu: Je! kizazi kitakacho kuwepo katika kipindi hicho kitaishi katika mazingira ya namna gani?.Hakika hatua za dhati zinahitajika kukomesha uharamia huu.

Kutokana na kukithiri kwa uvuvi usio kuwa WA kitaalamu,uchafuzi wa mazingira, kuongezeka kwa joto katika bahari, kina cha maji baharini kupungua, kuharibika kwa matumbawe na upotevu mkubwa wa mikoko hii yote ni hatari kubwa kwa mazingira.

Hata hivyo takwimu nyingine zinaonesha kuwa mabadiliko haya yamesababisha hasara kubwa kwa mazingira yetu, ikiwa ni pamoja na mito mingi kukauka, hii ni hali ya hatari kwa sababu uhaba wa maji ni janga la dunia nzima.

Uchafuzi unaofanywa katika miji yetu nao umekuwa ni tatizo kubwa kwani inakadiriwa kuwa takribani tani 10,000 za taka ngumu zinazalishwa kila siku nchini kote na asilimia kati ya 80 hadi 90 ya taka hizo hazizolewi.

Mabadiliko haya ya tabia nchi yamekuwa ni changa moto  kubwa kwani yanagusa kila sekta na makadirio ya haraka yanaonesha kuwa nchi yetu inahitaji kwa uchache dola milioni 150 mpaka 500 ili kubaliana na hali hii ya mabadiliko ya tabia nchi.

Katika mkutano huo uliofanyika nchini Swiden ujumbe ulilenga katika kuelimisha na kuihamasisha jamii kuchukua hatua zinazo lenga kuhifadhi mazingira.

Hii ililenga sehemu muhimu kama , uhifadhi wa misitu ya asili, upandaji miti, hifadhi ya vyanzo vya maji, maziwa , mito na mabwawa na mambo mengine yote yanayoendana na  mabadiliko ya tabia nchi.

Katika miaka ya hivi karibuni Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na Serikali ya Norway ambayo imetoa takriban dola milioni 100 katika kipindi cha miaka mitano ijayo imekuwa mstari wa mbele kupambana na hali hii.

Vilevile Tanzania imeanza kutekeleza mpango wa taifa wa kuhifadhi misitu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kupitia mauzo ya gesi joto inayonyonywa na misitu.

Katika kutekeleza mpango kama huum, tayari wilaya kama Bagamoyo, Kilolo na Mufindi zimeahinishwa kama ni wilaya za majaribio katika mpango huo,wakati  Zanzibar tayari mipango kazi imeshaanza.

Vilevile katika mkutano huo wa mazingira Umoja wa Mataifa ulitangaza mwaka huo kuwa ni mwaka wa kimataifa wa Bioanuai, ujumbe ni “biodiversity is life; biodiversity is our life” yaani biounuai ni uhai.

Hapa tunaona kwa namna gani ujumbe huu ulivyolenga katika kuhamasisha ushiriki wa Jumuiya za Kimataifa katika kuhifadhi bionuai kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika kukabiliana na matatizo haya taasisi zote, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali na wananchi wote kwa ujumla yatumie maadhimisho haya yanayo adhimishwa kila mwaka kuchukua hatua za dhati kukabiliana na matatizo haya.

Kamati zote za mazingira kuanzia ngazi za vijiji zitumie fursa hii kuanza kutoa elimu na kuhamasisha jamii nzima juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu kwa ajili ya leo na kesho.

Katika kutekeleza hatua hizi wananchi wanayo nafasi ya kuchagua ni mambo gani ya kufanya ili kuweza kutekeleza shughuli za utunzaji wa mazingira na kuendelea na shughuli zao za kila siku za kimaendeleo.

Kwa upande wa serikali, licha ya kujitahidi kuja na mipango na mikakati ya kuweza kuliokoa taifa na majanga haya ya mabadiliko ya tabia nchi, lakini bado juhudi za dhati zinahitajika ili kuweza kuifikisha elimu husika kuanzia ngazi ya kaya, kijiji, wilayani na hadi ngazi ya taifa.

Serikali kuanzia ngazi za vijiji mpaka taifa ihakikishe kuwa pana kuwepo kwa udhibiti wa shuguli za kibinadamu ambazo ni hatarishi kwa mazingira.

Hii ni kazi inayohitaji ushirikishwaji wa wananchi wote bila ya shuruti kwani uharibifu huu mkubwa unaozidi kushika kasi una madhara kwetu sote bila kujali tofauti zetu  kimapato, kidini, kisiasa au kijinsia.

Pawepo na sheria kali zitakazo weza kuwaogopesha wananchi juu ya uharibifu huu kuanzia katika misitu, vyanzo vya mito, maziwa, hifadhi na kwingine kote.

Hali hii kwa kiwango kikubwa iendane na upandaji  miti katika maeneo ambayo tayari yameshakuwa jangwa hii itasaidia kuanza kuirejesha Tanzania na dunia nzima mahali salama

Na mwisho naomba nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kwa Watanzania wote kwa ujumla kwa kuwahimiza kujitahidi kuyahifadhi mazingira yetu ili yatutunze kwani hili ni jukumu letu sote   na hii ni kwa manufaa ya Tanzania ya leo na kesho.


No comments:

Post a Comment