21 November 2012

CHADEMA kuwajengea uwezo viongozi wao kupitia mafunzo


Na Kassim Mahege

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinajipanga kutoa mafunzo ambayo yatawajengea uwezo viongozi mbalimbali wa chama hicho nchi nzima wakiwemo Wenyeviti na Makatibu kama hatua moja wapo ya muendelezo wa Operesheni ya
Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).


Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa chama hicho,
Bw. Benson Kigaila, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema chama hicho kinaendelea kujiimarisha kwa kutekeleza mikakati ya M4C yenye lengo la kuleta uongozi bora, kueneza
sera sahihi, kutengeneza mikakati makini pamoja na kujenga
oganaizesheni thabiti katika ngazi zote.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo ya siku mbili yamepangwa kuanza Novemba 22-23 mwaka huu, ambayo yatatolewa darasani na baada ya hapo, watafanya mafunzo ya vitendo.

“Makatibu na Wenyeviti wa mikoa watasambaa kushambulia vitongoji na vijiji vyote vya Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo hayo.

“Mafunzo ya darasani na yale ya vitendo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya ujenzi na uimarishaji chama hiki hasa kupitia M4C ambayo moja ya malengo yake ni kuwajengea uwezo  viongozi  wetu,” alisema Bw. Kigaila.

Alisema mafunzo hayo pia yatawahusisha viongozi wa kitaifa na watendaji wa Makao Makuu na yatafanyika wilayani Karagwe, mkoani humo kwa kushirikisha watu 64 kutoka mikoa yote 32.

Bw. Kigaila aliongeza kuwa, Wenyeviti na Makatibu wa mikoa
yote nchini watafanya mikutano ya ndani na ile ya hadhara katika Wilaya nzima ya Karagwe ambayo ina majimbo mawili ambayo ni Karagwe na Kyelwa, yenye kata 41.

“Katika kutekeleza mafunzo haya, tutafanya mikutano yetu kwa kasi ile ile kama ilivyokuwa kwenye M4C, katika mikoa ya Mtwara na Morogoro,” alisema Bw. Kigaila.

Alisema lengo moja wapo la M4C ni kuwajengea uzoefu
viongozi wao ili waweze kukitumikia chama kwa umakini zaidi.

No comments:

Post a Comment