22 November 2012

Vijana watakiwa kujitokeza kutoa maoni ya katiba mpya


Na Jesca Kileo

KATIBU wa Mkoa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Vyuo vya Elimu ya Juu, Bw.Christopher Ngubiagai ametaka vijana wasomi wa mkoa huo kutokubali kulishwa maneno na badala yake wajitokeze kwa wingi kutoa maoni juu ya upatinaji wa Katiba Mpya ya Tanzania.


Alisema hali hiyo itasaidia kupatikana kwa Katiba itakayolenga mambo muhimu ambayo yatalifanya Taifa kuwa imara na lenye nguvu za kiuchumi, utulivu wa kisiasa na utamaduni wa kitanzania kwa kuzingatia mfumo wa elimu yetu.

Akizungumza jana na waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu huyo alisema upatikanaji wa maoni bora utasaidia kutengenezwa kwa Katiba itakayoonyesha ulinzi wa rasilimali zetu.

Bw.Ngubiagai alisema kijana msomi akikubali kutumiwa na kupandikizwa maoni haitasaidia bali atakuwa ni miongoni mwa watu watakaoliletea matatizo Taifa hasa kutokana na kupatikana kwa Katiba isiyotokana na mawazo ya watu.

"Tunaitaka Katiba itakayosimamia rasilimali ardhi yetu, kulinda haki za makundi ya kijamii hasa vijana pamoja na kuleta amani, udugu na ujamaa,"alisema Ngubiagai.

Alisema kupambanua haya lazima watumie uwepo wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndani ya mkoa wa Dar es Salaam kutoa maoni yao vijana wasomi kutumia muda huu vizuri.

Bw.Ngubiagai alisema vijana wasomi watumie muda wao vizuri kutoa maoni kwa kuwa katiba hiyo ni kwa asilimia kubwa ni yao kwa kuwa wana umri mrefu wa kuishi na wakiitendea haki kwa kutoa maoni endelevu itawalea na kuwatunza vema.

Kutokana na hali hiyo Katibu huyo aliwataka viongozi wa matawi yaliyopo ndani ya taasisi ya vyuo vikuu nchini kuhakikisha wanafahamu vizuri maudhui ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano iliyopo sasa ili waweze kuwa na wigo mpana wa kutoa maoni yao.

Alisema kuwezekana kwa jambo hilo kutasaidia kutolewa kwa maoni bora na yenye mwelekeo wa kuisaidia Taifa hasa kutokana na wasomi kuwa chachu na fikra mpya ya mageuzi nchini.

Aidha alitoa wito kwa vijana wote wasomi kutoa maoni yao yatakayosaidia kulifanya Taifa kuwa  imara lenye nguvu za kiuchumi,utulivu wa kisiasa na utamaduni wa kitanzania kwa kuzingatia mfumo wa elimu yetu.




1 comment:

  1. JUKWAA LA KATIBA NDILO LIMEKUWA KIRANJA WA TUME YA KUKUSANYA MAONI YA KATIBA MPYA VIJANA WENGI WAMEJAZWA MATANGO PORI WALA HAWANA LA KUCHANGIA LABDA MUWAITE JUKWAA LA KATIBA WATOE MAONI YAO ILI WAWAACHE HURU WATANZANIA ILI WATOE MAONI KULINGANA NA MAZINGIRA YAO

    ReplyDelete