22 November 2012

Wazee watakiwa kukemea vijana kukaa vijiweni


Na Stella Shoo,
Morogoro.

WAZEE wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro wameshauriwa kukemea tabia ya vijana na watoto wao kukaa vijiweni na kunywa pombe bila kujishughulisha na uzalishaji,kwani tabia hiyo haitaweza kutokomeza umaskini unaoikabili jamii wilayani humo.


Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Uhusiano wa Taasisi ya MOROPEO, Bw. Wilson Kaluwesa alipokuwa akitoa mada katika warsha ya siku tatu iliyoanza jana kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuhusu changamoto zinazowakabili wazee wilayani humo.

Alisema ili umaskini miongoni mwa jamii upungue , tabia ya vijana kukaa vijiweni bila kujishughulisha na uzalishaji ipigwe vita kwa nguvu zote na vijana wahimizwe kujiunga na vikundi vya uzalishaji.

Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Rudewa, Bw. James Mng’hondwa alisema kuwa pamoja na kuwa wazee wana matatizo mbalimbali, lakini matatizo mengine  wanajitakia wao wenyewe kwa kuwa wanawajengea watoto au vijana wao mazingira ya kubweteka jambo linalowapa wazee wakati mgumu wa kushughulikia familia huku wakiwa hawana nguvu badala ya vijana ama watoto wao kufanya shughuli hizo.

“Wazee wana wakati mgumu ndio, lakini hata wazee wa pia wanajijengea wakati mgumu wao wenyewe kwa kuwa hawana desturi ya kuwajengea mazingira ya kujishughulisha vijana ama watoto wao,hivyo vijana wengi ama watoto wao kwenda kushinda vijiweni wakinywa pombe pamoja na kucheza kamari jambo linalowafanya washindwe kumudu hali ya maisha yanayowakabili,”alisema Bw. Mng’hondwa.

Akifafanua zaidi, Bw. Mng’hondwa alisema kuwa pamoja na changamoto hizo, lakini pia wazee pamoja na wazazi wanatakiwa kuwaelimisha watoto wao madhara ya kuwa na mimba zisizotarajiwa

Alisema wazee hao ndio wanaachiwa watoto hao wawalee na kuwasababishia watoto hao maisha magumu na mazingira hatarishi jambo linalowapa wazee hao wakati mgumu.
1 comment:

  1. WAZEE WASILAUMIWE ELIMU ITOLEWAYO INAWAANDAA VIJANA KUAJIRIWA HAKUNA TOTAUTI NA ENZI ZA MKOLONI TATIZO TULIPOONDOA AZIMIO LA ARUSHA HATUKUFIKIRI MBELE YA PUA ZETU KWANI HATUKUJUA KUWA SERA YA ELIMU NAYO ILITAKIWA KUBADILISHWA KAMA SIASA YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA IMMEPIGWA CHINI JE ELIMU YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA ITAKUWEPO SERIKALI IWEKE SERA MPYA YA ELIMU BILA HIVYO NI MAKOSA KULAUMU WAZEEE

    ReplyDelete