21 November 2012

Jina la Katibu Mkuu Kilimo sasa latumika kutapeli watuNa Mariam Mziwanda

WIMBI la utapeli wa kutumia majina ya wakubwa serikalini, sasa limeshika kasi na kuibukia katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika baada ya baadhi ya watumishi wa taasisi zilizopo chini
ya Wizara hiyo, kunusurika kutapelewa.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohamed Muya, aliyasema
hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa
harai na kutumia fursa hiyo kuuhadharisha umma juu ya utapeli
huo ambao umehamia katika Wizara yao.

Alisema matapeli hao wamefanikiwa kutumia jina lake katika matukio mbalimbali ambapo hadi sasa, wamejipatia sh. milioni
nane, kati ya hizo sh. milioni tatu walipewa na Ofisa Kilimo na
Mifugo wa Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga.

Walisema sh. 500,000 walizipata kutika Taasisi ya Kilimo Uvinza,  ambapo matukio yote yalilihusisha jina lake kwa madai ya kutoa maagizo kwa Maofisa hao watume pesa haraka.

“Naomba kuuhadharisha umma ujihadhari na matapeli hawa ambao wamekuwa wakitoa maagizo kwa watu mbalimbali kuwa Kamati za Wizara yangu zimekwama kwenye baadhi ya mambo hivyo kuomba msaada wa fedha pamoja na kuwapigia simu viongozi wa kanda mbalimbali wakiwataka watume fedha haraka,” alisema.

Alisema pia matapeli hao wamekuwa wakipiga simu sehemu mbalimbali na kudai Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alikuwa
safari na kupata ajali hivyo hivyo zinahitajika fedha za haraka.

“Jamani pesa za Serikali hazitolewi kirahisi namna hiyo bali kuna utaratibu wake wa kuzitoa, Wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara hii na watumishi wengine nawaomba mtekeleze kazi zenu
kwa kufuata misingi na sheria ili kukomesha utapeli huu,” alisema.

Bw. Muya alisema matukio hayo yametingisha kwa Meneja wa Kanda wa NFRA-Arusha, Makambako, Longido na Pangani
ambapo baadhi yao wamenusurika na wizi huo baada ya kufanya
mawasiliano ya moja kwa moja na ofisi yake.

Alisema matapeli hao hutumia namba 0757-813317, ambapo anayepiga simu hujitambulisha kwa jina la Bw. George Lubeleje ambaye ni mbunge wa zamani wa Mpwapwa, mkoani Dodoma.

Aliongeza kuwa, matapeli hao wanapopiga simu kwa wahusika, hutua maelekezo ya fedha hizo kutumwa katika namba 0766-487181 kwa madai ndiyo inayotumika kutatua tatizo husika na baada ya kupatiwa fedha hizo, simu hiyo huwa haipatikani tena.

Alisema tayari amefanya mawasiliano na Bw. Lubereje ambaye naye ameonesha kushangazwa na matukio yaliyofanywa na matapeli hao wakilihusisha jina lake.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Wizara hiyo, Bw. Ernest Doriye, alisema kutokana na matukio yanayoendelea juu ya Bw.
Muya tayari wameanza kuchukua hatua za kisheria.

“Lengo ni kukomesha utapeli huu ambapo uchunguzi wa awali umebaini namba ambayo matapeli huitumia na kujitambulisha
wao ni Bw. Lugereje, imesajiliwa kwa jina la Said Mkumba.

Alisema hivi sasa wanaendelea na uchunguzi kwa ajili ya
hatua zaidi za kisheria wakihusisha mamlaka mbalimbali.

Hivi karibuni, matapeli hao wameendelea kuitikisha nchi hasa katika Ofisi za Serikali, ikiwemo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi baada ya kutumia jina la Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Bw. Philipo Mulugo, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutumia jina la Balozi Khamis Kagasheki na taaasisi nyingine mbalimbali.


No comments:

Post a Comment