21 November 2012

Tume ya Katiba yamalizia mikutano yake


Na Darlin Said

TUME ya Mabadiliko ya Katiba, jana imeanza mikutano ya kukusanya maoni katika mikoa sita ukiwemo Dar es Salaam
ambayo itamalizika Desemba 19 mwaaka huu.


Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu, Joseph Warioba aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Arusha,
Simiyu, Geita, Mara na Mjini Magharibi.

Alisema katika mikoa hiyo, wamepanga kufanya mikutano miwili kila siku isipokuwa Mkoa wa Dar es Salaam itafanyika mikutano minne ambayo itaanza saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana na kuendelea saa nane mchana hadi 11 jioni.

Aliongeza kuwa, taratibu zote za kukusanya maoni katika mikoa hiyo zimekamilika ambapo wajumbe wa tume na watumishi wa Sekretarieti wamejipanga katika makundi saba.

“Kila Mkoa kutakuwa na kundi moja isipokuwa Dar es Salaam kutakuwa na makundi mawili, Januari 7,2013 tume hii itakutana
na asasi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia, kidini, vyama vya kitaaluma, wakulima, wafanyakazi na wadau wengine wakiwemo wenye uzoefu katika masuala mbalimbali.

Awali Jaji Warioba alisema, tume hiyo imerizishwa na kazi inayoendelea na wananchi jinsi wanavyojitokeza kutoa maoni yao.

Aliongeza kuwa, katika awamu ya tatu ya ukusanyaji maoni ya Katiba Mpya idadi ya wananchi imezidi kuongezeka ukilinganisha na awamu ya kwanza na pili.

“Tayari tumefanya mikutano 522 katika mikoa tisa ingawa tulipanga kufanya mikutano 496 lakini kutokana na uwepo wa mahitaji mapya kwa wananchi, tume iliamua kuongeza idadi ya mikutano ili kuwapa fursa zaidi.

“Katika awamu ya tatu, wananchi 392,385 walihudhuria mikutano ambapo watu 21,512, walitoa maoni kwa kuzungumza wakati na 84,939 kwa maandishi, 1,639 walitoa kwa kuzungumza na maandishi, alisema Jaji Warioba.

Alisema mwitikio wa wananchi katika kutoa maoni umekuwa wa amani, utulivu na kusikiliza wanavyoelekezwa ambapo hali ya wananchi kutoa maoni waliyomezeshwa na vikundi, taasisi na
vyama vya siasa imepungua.

Wakati huo huo, Jaji Warioba alidai kusikitishwa na zinazotolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Bw. Deus Kibamba kuwa tume hiyo inafanya kazi zake kwa kuripua.

“Changamoto zote anazozisema Bw. Kibamba sisi tuliziona tangu mwanzo na tumejipanga kuzikabili hivyo tume inafanya kazi kwa kuzingatia sheria si matakwa yake,” alisema Jaji Warioba.

No comments:

Post a Comment