21 November 2012

Askari Pori la Kijereshi wadaiwa kuua mfugaji kwa kumpiga risasi


Na Raphael Okello, Busega

ASKARI wa Pori la Akiba la Kijereshi, lililopo katika Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara, wanadaiwa kuwashambulia kwa risasi wafugaji wa Kijiji cha Kijereshi, kumuua mmoja na mwingine kujeruhiwa vibaya.

Tukio hilo limetokea juzi saa 12 jioni, mita 30 nje ya eneo la
mpaka wa hifadhi hiyo na Kitongoji cha Muungano A.

Waandishi wa habari, Diwani wa Kata ya Mkula na baadhi ya viongozi wa Serikali ya kijiji hicho, jana walitembelea eneo la
tukio na kushuhudia damu na maganda matatu ya risasi ambayo
yalikuwa nje ya eneo la hifadhi hiyo.

Inaelezwa kuwa, maganda mengine manne ya risasi yaliokotwa na askari upelelezi wa Jeshi la Polisi wilayani Busega ambao walifika eneo la tukio jana asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Hositali ya Mkula wilayani humo, mmoja kati ya wachungaji aliyejeruhiwa kwa
risasi mbili miguuni, Bw. Masangu Masake, alisema askari wa
hifadhi hiyo waliwavamia wakati wakichunga kando ya hifadhi
na kuanza kuwashambulia kwa risasi.

“Mimi nilipigwa risasi mbili miguuni, pia nilisikia milio mitatu
ya risasi ambazo zilipita juu lakini kaka yangu Bw. Kuyi Masake alipigwa risasi moja mgongoni na kutokea tumboni na nyingine ilipigwa kwenye paja,” alisema Bw. Masake.

Alisema baada ya kaka yake kujeruhiwa, askari hao walimchukua kwenye gari lao hadi Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (DDH), ambapo hali yake ilizidi kuwa mbaya hivyo alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza na jana alifariki
dunia saa 11 alfajiri.

Mkazi wa kijiji hicho ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema juzi saa 12 jioni akiwa nyumbani kwake, mita 200 kutoka mpakani mwa hifadhi hiyo, alisikia ngurumo ya gari ambayo
ilikuwa ikiendeshwa kwa kasi kubwa.

“Ghafla niliona gari hilo likifuata baadhi ya mifugo ambayo
ilikuwa nje ya hifadhi, baadhi ya askari walikuwa wakisema
kwa sauti 'simama, simama’.

“Baada ya hapo ilisikika milio ya risasi na kushuhudia askari wawili wakimbeba mfugaji mmoja aliyeanguka chini na kumingiza kwenye gari ambalo lilitokomea ndani ya hifadhi,” alisema.

Akiwa katika eneo la tukio, Diwani wa Kata ya Mkula, Idaso Mayala, alilaani kitendo hicho na kudai kuwa, askari hao pamoja
na kutenda kosa hilo hawakwenda polisi kuchukua fomu ya PF3.

Hadi jana, taarifa kutoka Hospitali ya Bugando, zilidai marehemu hajafanyiwa uchunguzi wowote ambapo ndugu zake na viongozi
wa Serikali ya kijiji hicho walihoji sababu za uchunguzi huo kuchelewa lakini hawajapewa majibu yoyote.

Hadi sasa Jeshi la Polisi linashikilia askari wawili wa hifadhi hiyo ambapo Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi, alikiri kutokea kwa hilo na kudai kutoa taarifa zaidi baadaye.

Naye Kamanda wa Hifadhi ya Pori ya Kijereshi, aliyejitambulisha kwa jina moja la Munishi, alipoulizwa kwa simu juu ya tukio hilo alikiri askari wake kuhusika na uchunguzi zaidi unaendelea.

No comments:

Post a Comment