23 November 2012

Thabo Mbeki: Viongozi Wazee chanzo cha umaskini TZ




Na Grace Ndossa

RAIS mstaafu wa Afrika Kusini, Bw. Thabo Mbeki, amesema Tanzania imeshindwa kupiga hatua ya maendeleo kwa sababu ya viongozi wenye umri mkubwa kuendelea kung'ang'ani madaraka.


Alisema pamoja na mipango mizuri ya maendeleo iliyopo nchini tatizo kubwa lililopo ni utekelezwaji wake.

Rais Mbeki aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kukutana na viongozi mbalimbali na wafanyabiashara ili kujadili changamoto zinazolikabili bara la Afrika.

“Tatizo la Tanzania kushindwa kupiga hatua ya maendeleo ni kutokana na viongozi kuendelea kung'ang'ania madaraka, kushindwa kutekeleza mipango na mikakati iliyowekwa.

“Katika kipindi cha uongozi wangu nchini Afrika Kusini, nilitembelea nchi nyingi na kujionea jinsi zinavyopiga hatua za maendeleo,” alisema Rais Mbeki.

Aliongeza kuwa, viongozi wa Tanzania wanapaswa kutekeleza mipango waliyonayo kama nchi nyingine ili Taifa liondokane na umaskini uliopo kufikia malengo yaliyopo.

Rais Mbeki alisema Tanzania ina mipango mizuri katika sekta ya kilimo lakini utekelezwaji wake ndio tatizo.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiamo wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira, njaa, migogoro ya kidini, magonjwa kwa sababu ya Serikali kutochukua maamuzi magumu.

Alisema uongozi una nafasi yake ambapo viongozi bora ni wale wanaotekeleza mipango mikakati na kutimiza sera waliyojiwekea.

Naibu Waziri wa Sayansi na Tekinolojia, Bw. Januari Makamba alisema uongozi wa kuachiana madaraka utasaidia kuleta
mabadiliko katika nyanja mbalimbali.

Alisema umefika wakati wa Tanzania kujipanga na kuweka mfumo mzuri wa uongozi, uchaguzi na mgawanyiko wa rasilimali na taasisi zilizopo ziwe imara katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

Naye Jaji mstaafu, Joseph Warioba, alisema kipindi cha nyuma vijana ndio waliohusika kushughulikia ukombozi na kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.

“Hivi sasa tatizo lililopo, wazee waliopo madarakani ni wagumu kuwaachia vijana madaraka ndio maana hatuwezi kutoka hapa tulipo,” alisema Jaji Warioba.

5 comments:

  1. Mbeki ameongea kweli. Na si kwa viongozi wazee tu, hata sera zilizozeeka pia. Uongozi wa Serikali ni kwa mazoea na mabadiliko ni vigumu kweli kufanyika. Kiukweli, ukichunguza undani wa ugumu wa utekelezaji wa sera, hasa za chama tawala, unatokana na itikadi za makada wazee wasiokubali mabadiliko, ambapo viongozi vijana wamekuwa wakishindwa kufanya mambo mazuri wanapopewa nafasi na kujikuta wamebanwa na itikadi za wazee hawa, hivyo kujikuta wanaimba nyimbo zilezile zisizo na waitikiaji!

    ReplyDelete
  2. Ni vigumu kuamini kuwa maneno haya pia yametoka kinywani mwa Jaji Joseph Warioba! ambaye anayo nafasi ya kumshauri rais kuacha kuteua watu walikwisha staafu kwenye nafasi mabalimbali za kufanya maamuzi! kitendo ambacho kinaligharimu taifa. Maana kuweka watu waliostaafu au hata wanaokaribia kustaafu kwenye nafasi za maamuzi ni kuliumiza taifa kwa sababu wao wanakuwa tayari wamechoka na wengi hufanya kwa mazoea huku wakisubiri siku zao ziishe. Nimefurahishwa sana na mawazo haya ya Rais Msitaafu wa Afrika Kusin Mheshimiwa Thabo Mbeki.

    ReplyDelete
  3. MBEKI SIMWAMINI SANA ALIYENG'ATUKA KWA HESHIMA NI MZEE MANDELA YEYE ALIMWEKEA ZUMA MIZENGWE KESI ZA KUSINGIZIWA KIKO WAPI ZUMA YUKO IKULU WALA HANA HAJA YA KULIPIZA KISASI SIASA ZA TANZANIA NI ZA KUCHAFUANA VISASI WAKO RASILIMALIWATU KAMA DR SALIM AHAMED SALIM KUTOKANA NA SIASA CHAFU HATAKI SIASA WAKATI ANA CV KALI SANA

    ReplyDelete
  4. YEYE AMELETA NINI HUKO SOUTH? HALI ILIKUWA MBAYA WAKATI WA UONGOZI WAKE MPAKA AKAFUKUZWA URAIS. WANATAMBIA TU UCHUMI NA MIUNDO MBINU ILIOWEKWA NA MAKABURU.HUO NDIO UKWELI

    ReplyDelete
  5. HIVI NI NANI ANANG"ANG'ANIA MADARAKA KAULI HII ANGEITOA ZIMBABWE NINGEMWELEWA SINA UHAKIKA KWA KUWA OBAMA NI RAIS KIJANA BARAZA LAKE LA MAWAZIRI WOTE NI VIJANA HUYU MZEE KAFILISIKA KISIASA MBONA HUKO AFRIKA YA KUSINI KAMA WANAWAENZI VIJANA MBONA MWENYEKITI WA VIJANA WA ANC MALEMA ANABANDIKIZIWA KESI ZA BANDIA SAWA NA UTAWALA WA MBEKI KWA ZUMMA AKATAFUTE KITI CHA UVIVU AKALIE HANA JIPYA

    ReplyDelete