23 November 2012

Nipo tayari kuitumikia CCM kimwili, kiakili


Na Mwandishi Wetu, Rukwa

KATIBU Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana, amesema yupo tayari kimwili na kiakili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ili kuwasidia Watanzania.

Bw. Kinana aliyasema hayo mjini Rukwa jana katika mkutano wa hadhara ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku nne aliyoianza juzi katika mikoa ya Mtwara, Rukwa, Geita na Arusha.

“Awali nilitangaza kustaafu siasa kwa sababu nimeshika kwa muda mrefu nyadhifa za kuchaguliwa nikaona hakuna sababu ya kusubiri hadi nichoke ndio niondoke lakini baada ya maamuzi yangu, Rais Jakaya Kikwete (Mwenyekiti wa CCM Taifa), akaniteua katika nafasi hii ili nikisaidie chama.

“Kwa mtu mwenye hekima na uadilifu, unapoteuliwa na Mwenyekiti wa chama chako tena kinachotawala, lazima ukubali bila kinyongo hivyo nikakubali sasa napenda kuwaambia kwamba, nipo tayari, kimwili, kiakili kuhakikisha nawatumikia wana CCM na
Watanzania kwa weledi na ufanisi mkubwa,” alisema.

Akizungumzia mikakati ya utekelezaji wa kazi zake, Bw. Kinana alisema atajikita zaidi katika kuimarisha uhai wa chama kwenye ngazi za mashina, matawi na kufafanua kuwa azma hiyo kimsingi sio yake ila ya CCM.

“Nataka niwaambie kwamba, kazi muhimu na ya lazima ambayo viongozi wote tunapaswa kuifanya kwa pamoja na umakini mkubwa ni hii ya kukijenga kujenga chama katika ngazi za mashina na matawi, hili si langu bali ni maamuzi ya Mkutano Mkuu wa
CCM uliomalizika mjini Dodoma hivi karibuni,” alisema.

Alisema hakuna miujiza itakayokiinua chama hicho zaidi ya kuimarisha uhai wa mashina, matawi ambapo kutokana na
umuhimu huo ndio maana ameanza ziara za kukabua uhai
wa chama na kuwataka viongozi wa ngazi zote wa
CCM kufuata nyayo zake.

Katika ziara hiyo Bw. Kinana ambaye anafuatana na Makatibu wa NEC, Bw. Nape Nnauye (Itikadi na Uenezi) na Bw. Mohamed Seif Khatib (Oganaizesheni), pamoja na baadhi ya Mawaziri akiwemo Naibu Waziri wa TAMISEMI, Bw. Aggrey Mwanri.

Katika mikutano hiyo amekuwa akikagua uhai wa matawi na mashina, kufanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero
mbalimbali za wananchi.

Akiwa mkoani Mtwara, Bw. Kinana alitoa fursa kwa wananchi kueleza kero inayohusiana na zao la korosho ambapo Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, ilibidi apande jukwaani kufafanua hali ya pembejeo za kilimo cha zao hilo, changamoto zake na namna Serikali inavyojaribu kuzitatua.

Mhandisi Chiza pia alizungumzia suala la wakulima wa zao hilo kucheleweshewa malipo yao.

Bw. Kinana alizungumzia kwa kina suala la pembejeo hasa mbolea ya Minjingu ambayo kama ilivyokuwa mkoani Mtwara, wananchi walilalamika na kudai kuwa haiwawezeshi kupata mazao ya
kutosha na kutaka ibadilishwe.

1 comment:

  1. NAKUBALIANA NA MADAI WAPO WANASIASA HAWATAKI KUNG'ATUKA WEWE KINANA ULISEMA UNASTAAFU MAMBO YA SIASA KILICHOKURUDISHA NI NINI??? SASA HIVI UNAFANYA KAZI ZA KATIBU MWENEZI HIVI UTAWEZA KUTENGUA UTEUZI WA MAWAZIRI WA KIKWETE AKILINI MWA KIKWETE RAIS MTARAJIWA NI ASHAROSE MIGIRO JEE ANA UBAVU WA KUMNADI YETU MACHO TUSUBIRI 2015

    ReplyDelete