19 November 2012
TAZARA kwafukuta, mazungumzo yakwama
Rehema Maigala na Rose Itono
MAZUNGUMZO ya kutafuta ufumbuzi wa mgomo wa wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) kati ya Wizara ya Uchukuzi na Menejimenti ya shirika hilo, yameshindwa kufikia muafaka hivyo kusababisha mgomo kuingia siku ya nne.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Tawi la TAZARA Mkoa, Bw. Musa Joseph alisema juzi saa mbili usiku viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (TRAWU) walipokea simu kutoka wizarani kuwataka wafike kwenye kikao ili kujadili madai yao.
Aliongeza kuwa, mazungumzo hayo yaliitishwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi Dkt. Charles Tizeba, ambapo viongozi wa TRAWU hawakuweza kufika kwa kuhofia usalama wao.
“Mkutano huo ulihudhuriwa na Menejiment ya TAZARA na Naibu Waziri ambao hadi saa saba usiku, hawakuweza kufikia muafaka.
Alisema jana asubuhi viongozi wa TRAWU na Menejimenti ya TAZARA waliendelea na mazungumzo ili kujua ni wapi pesa za kuwalipa wafanyakazi mishahara ya miezi miwili zitapatikana na kuwezesha huduma za usafiri kurejea kama kawaida.
Naye mfanyakazi wa TAZARA, Bw. Amri Hussein, alisema tatizo ambalo limesababisha shirika hilo kufikia hatua hiyo ni uundo wake kisheria unaosema lazima Mkurugenzi wa shirika atoke Zambia na Msaidizi wake awe Mtanzania.
“Sheria husika inambana Mkurugenzi Msaidizi kwa kumnyima madaraka, kazi ya huyu Mkurugenzi ni kumshauri Mkurugenzi Mkuu si vinginevyo.
“Hali hii inamnyima madaraka kabisa Mkurugenzi Msaidizi hivyo kushindwa kuchukua hatua yeyote hata kama kuna kosa limefanywa na Mameneja,” alisema Bw. Hussein na kuishauri Bodi ya shirika hilo kuibadilisha sheria hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Uchukuzi, Lisso Biseko alipoulizwa kuhusiana na kikao kilichowahusisha TRAWU, Menejimenti ya TAZARA na Wizara, alikiri kuwa kikao hicho kinaendelea ili kujua hatma ya madai hayo na kurejesha huduma kama kawaida.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment