15 November 2012
Simba wamtafuta 'mchawi' *Uhuru kutua Azam, Owino Simba
Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa klabu ya Simba umelitaka benchi nzima la ufundi kila mmoja kuwasilisha ripoti yake mara baada ya kumalizika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya timu yao kuvurunda, hivyo wametaka kujua kiini cha timu yao kufanya vibaya.
Simba ambayo tangu kuanza kwa ligi imekuwa ikiongoza ligi, ilijikuta ikiporomoka hadi nafasi ya tatu na uongozi wa ligi kuchukuliwa na Yanga wenye pointi 29, huku Azam FC ikishika nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi 24 na Simba wanapointi 23.
Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini alisema kila mmoja ametakiwa kuwasilisha ripoti yake kwa uongozi ili watakapokutana wazipitie zote na kujua tatizo ni nini.
"Tangu kumalizika kwa mzunguko wa kwanza mara kwa mara tumekuwa tukikutana na uongozi na kubwa zaidi wanataka kila mmoja kuwasilisha rioti yake ili wakikutana katika kikao cha Kamati ya Utendaji waweze kuzipitia zote," alisema kiongozi huyo
Alisema katika ripoti ya kocha wao mkuu Milovan Cirkovic pia atakuwa na mapendekezo yake ya nini kiboreshwe kwenye kikosi chake ili kurudisha upinzani mzunguko wa pili wa ligi.
Kiongozi huyo alisema kuna kasoro nyingi ambazo kocha atakuwa amegundua, hivyo kwenye ripoti hiyo itaeleza kila kitu, kwani kocha huyo amekuwa kimya bila kuzungumza na mtu juu ya safu ipi ifanyiwe marekebisho, hivyo amepanga katika ripoti yake ataweka kila kitu wazi.
Kamati ya Utendaji ya Simba inatarajiwa kukutana leo kwa ajili ya kuzungumzia ajenda mbalimbali mara baada ya kupitia ripoti kutoka benchi ya ufundi.
Wakati huo huo uongozi wa klabu hiyo umesema wamekubaliana na Azam FC kubadilishana wachezaji, ambapo George Owino atakwenda Simba na Uhuru Seleman kwenda Azam.
"Makubaliano ni ya asilimia 100 kwamba tumekubadiliana na wenzetu wa Azam kubadilishana wachezaji sisi tunamchukua George Owino na wao tutawapa Uhuru Seleman," alisema Msemaji wa Simba Ezekiel Kamwaga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment