21 November 2012

Rufaa ya TANESCO kwa Dowans Desemba 5



Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Rufaa Dar es Salaam, Desemba 5 mwaka huu inatarajiwa kuanza kusikiliza rufaa ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Dowans.


Rufaa hiyo namba 142/2012, inatarajiwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Nathalia Kimaro. Majaji wengine ni William Mandia na Katherine Oriyo.

Septemba 19 mwaka huu, TANESCO iliwasilisha mahakamani hapo rufaa ya kuomba zuio la utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu IliYowataka kuilipa Dowans zaidi ya dola za Marekani milioni 65.

Novemba 15,2011, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) chini ya Mwenyekiti wake, Bw. Gerald Aksen na wasuluhishi Bw. Swithin Munyantwali na Bw. Jonathan Parker, iliiamuru TANESCO iilipe Dowans fidia ya kiasi hicho cha fedha kwa kuvunja mkataba kinyume cha sheria.

Dowans ilisajiri tuzo waliyopewa na ICC ya kulipwa fedha hizo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaa ambayo iliiamuru TANESCO itekeleze amri iliyotolewa na ICC.


Hata hivyo, TANESCO waliwasilisha tena mahakamani hapo ombi la kuomba zuio la utekelezaji wa amri hiyo lakini Mahakama hiyo ilisema haina uwezo wa kusikiliza ombi hilo hivyo waliamua
kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

Katika rufaa yake, TANESCO inadai lengo la kufanya hivyo ni kuipa changamoto hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam, katika kesi namba 8/2011.

Inadai kuwa, kiwango ambacho TANESCO ipanaswa kuilipa Dowans ni kikubwa na kama italipa ni hasara kwake kiuchumi.

No comments:

Post a Comment