21 November 2012

Dkt. Slaa amgeukia Kikwete *Amtaka asitumie muda mwingi kushambulia upinzani


Na Queen Lema, Arusha

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, amemtaka Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete,
kutotumia muda mwingi kuvishambulia vyama pinzani.


Alisema Rais Kikwete anapaswa kutumia muda mwingi kutatua
kero za wananchi ili kupunguza ukali wa maisha unaowakabili
kwa sasa badala ya kukisema CHADEMA ambacho ni chama
makini kinakubalika na wananchi wengi.

Dkt. Slaa aliyesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha juu ya hoja mbalimbali ambazo zilizungumzwa katika Mkutano wa CCM uliofanyika Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Alisema katika mkutanmo huo, viongozi wengi wa CCM akiwemo Rais Kikwete alitumia muda mwingi kuelezea hatua za kuchukua ili chama hicho kiweze kukabiliana na vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Alisema CCM kinapaswa kutekeleza mikakati ya maendeleo ya wananchi ili waondokane na umaskini pamoja na kuboresha mazingira ya sekta mbalimbali hususan kutoa elimu bura
hasa ya sekondari ili kuwapunguzia wazazi mzigo.

“Juzi wakati natoka Dar es Salaam kuja Arusha, nilikutana na misururu mirefu ya mabasi ambayo yalibeba wanachama wa CCM ambao walikuwa wakienda katika mapokezi yake Mnazi Mmoja.

“Sikua kama Rais Kikwete anatambua kama wana CCM wenzake wanamdanganya kuwa chama chao kinapendwa kiasi gani maana haiwezekani wanachama watoke Mkoa mwingine ili kwenda kuongeza nguvu ya mapokezi yake,” alisema Dkt. Slaa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Slaa alidai kushangazwa na Rais Kikwete kwa kumteua Bw. Abdurahman Kinana kuwa Katibu
Mkuu wa CCM wakati anakabiliwa na kashfa mbalimbali.

Alisema Serikali ya chama tawala imejaa njaa, ufisadi na viongozi wake wengi wanakabiliwa na maovu mbalimbali ambapo safu mpya ya uongozi ndani ya CCM, haija jipya la kuweza kukizuia chama chao ambacho kinapendwa kutokana na sera zake.

“CCM kimeishiwa ubunifu, CHADEMA tuliibua sera ya elimu
bure katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010 leo hii chama tawala kimeibeba na kujifanya ya kwao, sisi hatuchukii bali waifanyie kazi ili wananchi waweze kunufaika,” alisema Dkt. Slaa.

Alisema ni wajibu wa CHADEMA kuibua changamoto mbalimbali za kiutendaji kwa chama tawala hivyo wataendelea kuzungumzia kasoro zilizopo hadharani hadi Serikali itakapoona umuhimu wa kutatua kero mbalimbali walizonazo wananchi.

No comments:

Post a Comment