19 November 2012

Polisi wazuia maandamano ya walimu Bunda


Na Raphael Okello, Bunda

JESHI la Polisi, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, limesitisha maandamano ya Chama cha Walimu nchini (CWT), wilayani
humo ambayo yalipangwa kufanyika leo.


Mkuu wa Kituo cha Polisi Bunda, ASP Mayunga Mayunga, alisema jeshi hilo limesitisha maandamano hayo kwa kuwa madai yote ya walimu nchini bado yanasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.

“Ieleweke kuwa, CWT tawi la Bunda ni sehemu ya CWT Taifa ambayo bado ina kesi na Serikali katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Kanda ya Dar es Salaam, wakidai masilahi mbalimbali hivyo kuwaruhusu maandamano ni kuingilia uhuru wa Mahakama,” alisema.

Mwenyekiti CWT wilayani humo, Bw. Francis Ruhumbika, alikiri kupokea barua ya polisi ya kusitisha maandamano hayo yenye namba BND/A.7/3/VOL.V/04 ya Novemba 13 mwaka huu na kuwataka walimu kuvuta subira kwa kutii agizo la jeshi hilo.

Hata hivyo, Bw. Ruhumbika alilishutumu jeshi hilo na kudai halijawatendea haki kwani madai ya walimu Bunda ni tofauti
na madai ya awali ya walimu nchini yaliyoko Mahakama Kuu.

Licha ya kuwataka walimu wilayani humo kutii agizo la polisi, alisema kitendo cha jeshi hilo kuzuia maandamano ya amani ni kuwanyima haki ya kikatiba.


“Ieleweke kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu Disheni ya Kazi ni inahusu walimu kuongezewa mishahara kwa asilimia 100, posho ya
ufundishia na ile ya mazingira magumu.

“Sisi madai yetu ni kulipwa mapunjo ya mishahara, madai yaliyohakikiwa, kurekebishiwa mishahara,hizi ni haki za
mtumishi zilizopo kisheria hazina uhusiano na kesi iliyoko mahakamani,” alisema Bw. Ruhumbika.

Aliongeza kuwa, halmashauri ya Bunda imeonesha nia ya
kutekeleza madai yao fikapo mwisho wa mwaka huu.

Kuzuiwa kwa maandamano hayo kumewakera baadhi ya walimu wilayani humo ambao wengine walianza kukodi magari kutoka vijijini ili kuungana na wenzao katika maaandamo hayo hadi
makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment