27 November 2012

Mvua za El-nino 'zayeyuka'Na Stella Aron

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imewahadharisha i wananchi kutumia maji kwa uangalifu na kuhifadhi malisho kwa ajili ya mifugo kutokana na mvua ndogo zilizonyesha hadi sasa.


Taarifa iliyotolewa na TMA kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, kuhusiana na mrejeo wa hali ya mvua za El-nino na La-nina, kipindi cha Julai na Novemba mwaka huu, imesema mabdiliko yaliyojitokeza si ya kawaida.

Ofisa Habari wa mamlaka hiyo, Bi. Monica Mutoni, alisema upo uwezekano wa kuwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa hivyo wananchi wanashauriwa kuendelea kuchukua tahadhari.

Alisema kipindi cha Julai hadi Septemba 2012, hali ya joto la bahari katika Ukanda wa Tropikali wa Bahari ya Pasifiki, iliongezeka na kuwa juu ya wastani hivyo kuashiria uwepo wa mvua hafifu za
El-Nino ambapo hali ya mifumo ya upepo, mgandamizo wa hewa katika usawa wa bahari na mawingu, vilishindwa kuwiana na ongezeko hilo hafifu la joto la bahari.

Aliongeza kuwa, mifumo ya upepo na mgandamizo wa hewa vimeendelea kusababisha upungufu wa unyevunyevu katika anga hivyo kusababisha hali ya mabadiliko ya joto la bahari na mifumo
ya hali ya hewa kuwa si ya kawaida na haijawahi kutokea katika miaka iliyopita.

Bi. Mutoni alisema kutokana na hali hiyo, taasisi zinazohusika na masuala ya hali ya hewa katika Kanda ya Pembe ya Afrika (ICPAC) na Kanda Kusini mwa Afrika (SADC-CSC) kwa mara ya kwanza zimeandaa warsha ya wataalamu wa hali ya hewa.

Katika warsha hiyo Tanzania ni miongoni mwa washiriki ili kufanya uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejeo wa mwelekeo wa mvua za msimu katika ukanda huo.
                                               
Kutokana na mabadiliko hayo, TMA imewashauri wananchi katika maeneo ambayo mvua inanyesha hadi sasa chini ya wastani,kutumia maji kwa uangalifu.

Alisema pamoja na mabadiliko yaliyojitokeza, upo uwezekano wa kuwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa.

No comments:

Post a Comment