27 November 2012

BTL, Levi Electronics wakabidhi zawadi kwa washindi wa ZUKU


Na Peter Mwenda

KAMPUNI ya Business Times Limited (BTL), kupitia gazeti lake la Majira kwa kushirikiana na Kampuni ya Wananchi, kupitia wakala wake Levi Electronics anayesambaza bidhaa ya ZUKU TV, jana wamekabidhi zawadi ya ving'amuzi na dish kwa washindi wawili
kati ya watatu wa shindano la “Shinda Biashara na Mtaji”.

Akizungumza kabla washindi hao hawajakabidhiwa zawadi zao, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Majira, Bw. Imma Mbuguni, alisema shindano hilo ni endelevu hivyo aliwataka wasomaji kuchangamikia fursa hiyo ya pekee ili kujikomboa kiuchumi.

Mshindi wa kwanza, Bw. William Kahale, alipata ving'amuzi 10 na dishi kwa idadi kama hiyo ambapo mshindi wa pili, Bw. Emmanuel Magabe, alipata zawadi ya seti tano za ving'amuzi na dishi kwa idadi kama hiyo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi zake, Bw. Kahale alisema hakutegemea kupata zawadi hiyo kwani pamoja na kushiriki shindano hilo hakuwa na imani kama angeshinda.

Kwa upande wake, Bw. Magabe, alisema aliahidi kulitangaza gazeti la Majira ambalo limemtoa katika umaskini na kuzingatia vigezo vya kuwapta washindi.

Washindi wote waliokabidhiwa zawadi zao jana wanatoka Dar es Salaam isipokuwa Bw. Muhaji Hassan ambaye ni mshindi wa tatu kutoka Zanzibar na atakabidhiwa zawadi yake hivi karibuni.

Mkuu wa Kitengo cha Usambazaji kutoka BTL, Bi. Sophia Mshangama, aliwataka washindi hao kuwa mabalozi wazuri wa kulitangaza Gazeti la Majira ili kuongesha idadi ya washiriki wanawake katika shindano lijalo.

“Tunaomba mkawashawishi wanawake huko muendako ili waandike michanganuo ya biashara katika shindano lijalo na kupata zawadi kama hizi kwani mkimuelimisha mwanamke mmoja, mtakuwa mmelialimisha Taifa zima,” alisema Bi. Mshangama.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Levi Electonics, Hatevele Mposo ambao ndio mawakala wa bidhaa ya ZUKU, alisema zawadi hizo
na nyingine zitaendelea kutolewa kwa Watanzania ili wapate nafasi ya kutumia chaneli zaidi ya 70.

No comments:

Post a Comment