21 November 2012

Mgimwa: Kuchelewa fedha za wahisani kunakwamisha miradi



David John na Jesca Kileo

WAZIRI wa Fedha, Dkt. William Mgimwa, amesema miradi mbalimbali iliyopo chini ya Wizara yake, haitekelezwi kwa
wakati kutokana na fedha za wahisani kuchelewa kuwafikia.

Alisema hivi karibuni alikutana na wadau wa maendeleo kutoka
nchi wahisani na kuwaeleza jinsi fedha wanazotoa zinavyotumika kwa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini.

Dkt. Mgimwa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa,
wahisani wamekuwa na msaada mkubwa kwa Tanzania
katika harakati zake za kupambana na umaskini hasa
kwenye sekta ya afya, barabara na elimu.

Aliongeza kuwa, pamoja na misaada inayotolewa na wahisani, Wizara hiyo bado ina changamoto kubwa ya kutozipata fedha
hizo kwa wakati na kufanya miradi mbalimbali iliyo chini ya
Wizara kuchelewa kuaza.

“Changamoto kubwa inayotukabili ni kucheleweshewa fedha ambazo Wizara inaziomba kutoka serikalini hivyo kusababisha
miradi ishindwe kutekelezwa kwa wakati, hali hii inachangia
tuchelewe kupiga hatua ya maendeleo,” alisema.

Dkt. Mgimwa alisema changamoto zipo nyingi na hasa katika
sekta ya afya ambako kuna ukosefu mkubwa wa dawa na waganga wakutosha na hasa katika zahati mbalimbali za Serikali nchini
hivyo kusababisha vifo kuongezeka.

Alisema sekta nyingine ni miundombinu ya barabara na elimu ambayo changamoto kubwa ni upungufu wa walimu, ubovu wa barabara mbali ya Serikali kujitahidi kuziboresha.

Hata hivyo Dkt. Mgimwa aliishukuru Serikali ambapo mwaka huu wa fedha waliomba fedha asilimia 60 na wakafanikiwa kupata zaidi ya hiyo kwa wakati muafaka hivyo kufanikiwa kutatua baadhi ya miradi ambayo ilikuwa haijaboreshwa.

Aliwaomba wadau hao wasichoke kuisaidia Serikali ili
iweze kufikia maendeleo wanayotarajia kuyafikia.

“Kupitia mkutano huu, tunazidi kuwaomba ndugu zetu waendelee kutusaidia, pamoja na changamoto hizi tunaamini kasi yetu ya kufikia maendeleo ni kubwa bila shaka tutafika,” alisema.

No comments:

Post a Comment